1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban ataka kusitishwa mapigano Yemen

Admin.WagnerD15 Juni 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- moon Jumatatu (15.06.2015) amefunguwa mazungumzo ya amani ya Yemen mjini Geneva kwa wito wa kusitishwa kwa mapigano chini ya misingi ya utu.

https://p.dw.com/p/1FhZU
UN Genf Friedensgespräche für Jemen Ban Ki-Moon
Picha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Zaidi ya watu 2,600 wameuwawa nchini Yemen tokea muungano wa nchi za Kiarabu unaoongozwa na Saudi Arabia kuanzisha operesheni za kijeshi hapo mwezi wa Machi kuwazuwiya waasi wa jamii ya Wahuthi wanaoungwa mkono na Iran kuingia katika mji wa Aden kumsaidia Rais Abd Rabuu Mansour Hadi wakati huo akiwa katika mji huo wa kusini kabla ya kukimbilia uhamishoni nchini Saudi Arabia.

Akizungumza na waandishi wa habari Ban amesema amesisitiza umuhimu wa kuwa na usitishaji huu mwengine wa mapigano kwa misingi ya ubinaadamu wa angalao wiki mbili.

Ban amesema "Ramadhani inaanza baada ya siku mbili.Ramadhani kwa jadi ni kipindi ambapo watu huombea amani,hutafakari na kuleta maelewano na usuluhishi.Kwa hiyo wananchi wa Yemen wanapaswa kufurahia amani ya aina hii."

Lakini mazungumzo hayo ya amani yanayodhaminiwa na Umoja wa Mataifa hayakuanza vyema baada ya Ban kukutana na wawakilishi wa serikali ya Yemen ilioko uhamishoni tu kutokana na kuchelewa kuwasili kwa ujumbe wa waasi.

Ujumbe wa waasi wakwama Djibouti

Ndege iliokuwa imewachukuwa wajumbe wa kundi la Wahuthi la Ansarullah na wale wa chama cha rais wa zamani wa nchi hiyo Ali Abdullah Saleh imebidi ituwe Djibouti baada ya kile kilichoelezwa kuwa kugoma kwa Misri kuipa ndege hiyo ruhusa ya kuruka kupitia anga yake.Ndege hiyo baadae imeruhusiwa kuondoka kuelekea Geneva.

Wafuasi wa waasi wa jamii ya Huthi nchini Yemen.
Wafuasi wa waasi wa jamii ya Huthi nchini Yemen.Picha: Reuters/K. Abdullah

Ban imebidi aondoke Geneva kabla ya kuwasili kwa ujumbe huo na kuyaacha mazungumzo hayo kwenye mikono ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Ismail Ould Sheikh Ahmed ambaye atakutana na ujumbe wa pande hizo mbili kwa nyakati tafauti kujaribu kuwashawishi waketi meza moja ya mazungumzo.

Uwezekano wa kusitisha mapigano

Waziri wa mambo ya nje wa Yemen Reyad Yassin Abdullah amefuta uwezekano wa kusitishwa kwa mapigano mara moja.

Wanajeshi wanaoiunga mkono serikali ya Rais Abd Raboo Mansour Hadi nchini Yemen.
Wanajeshi wanaoiunga mkono serikali ya Rais Abd Raboo Mansour Hadi nchini Yemen.Picha: picture alliance/dpa

Amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva usitishaji huo wa mapigano kwa ajili gani iwapo waasi hao wanaendelea kuikalia Yemen kwa mabavu, kuuwa watu watu wasiokuwa na hatia na kuangamiza kila kitu.

Hata hivyo amesema serikali yake inaweza kuzingatia usistishaji wa kiasi fulani wa mapigano iwapo Wahuthi wataodoka katika miji ikiwemo Aden na Taiz na kuwachilia huru wafungwa 6,000.

Mazungumzo hayo ya amani yanatarajiwa kudumu kwa siku mbili hadi tatu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AP

Mhariri : Iddi Ssessanga