Mazungumzo ya Syria yaingia awamu muhimu
27 Januari 2014Katika kile kinachoonekana kuwa ni ahadi ya kwanza kutolewa kwenye mazungumzo hayo, mpatanishi wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Lakhdar Ibrahimi, alisema hapo jana kwamba serikali imekubali kuwaruhusu wanawake na watoto kuondoka kwenye mji uliozingirwa wa Homs.
Kwa mujibu wa Brahimi, msafara wa mashirika ya misaada utaingia kwenye mji huo leo, akisema kwamba waasi na gavana wa huko tayari wamefikia makubaliano.
Brahimi, ambaye amekuwa akizungumza na kila upande peke yake, amesema kwamba amefurahishwa na hali inayoanza kujengeka kwenye mazungumzo hayo, ambapo kila upande unaonesha heshima kwa mwengine, lakini amekiri kwamba imekuwa vigumu kupiga hatua na pande hizo mbili zimekuwa zikienda taratibu mno kuelekea makubaliano ya amani.
Hata hivyo, ahadi hiyo ya serikali imepokea kwa hofu mjini Homs kwenyewe. Wanaharakati walio kwenye mji huo wamesema raia hawana imani na serikali na kwanza wanataka misaada ya kibinaadamu na hakikisho kwamba watakaoondoka kwenye mji huo hawatakamatwa.
Sehemu ya Mji Mkongwe ya Homs imezingirwa tangu mwezi Juni 2012, baada ya kuanzisha vuguvugu la upinzani dhidi ya serikali. Kiasi cha familia 500 zinaishi kwenye eneo hilo ambalo limekuwa likishambuliwa takribani kila siku.
Upinzani wang'ang'ania Assad aondoke
Msemaji wa upinzani kwenye mazungumzo ya Geneva, Louay Safi, amesema mazungumzo ya leo ndiyo yatakayoamua ikiwa serikali ya Assad iko tayari kwa suluhisho la kisiasa au inaendelea kung'ang'ania suluhisho la kijeshi.
Msemaji huyo amesisitiza kuwa "sasa muda umeshafika kuzungumzia kipindi cha mpito kutoka utawala wa kidikteta kwenda wa kidemokrasia."
Lakini upande wa serikali kwenye mazungumzo hayo umeshaondoa kabisa uwezekano wa kujadili kuondoka kwa Assad madakarani, na hadi sasa umekubali tu kuzungumzia masuala ya kibinaadamu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Faisal Mikdad, amewaambia waandishi wa habari kwamba serikali yake haina nia ya kuendelea na vikao vya muda mrefu, zaidi ya kumaliza vita dhidi ya ugaidi.
"Tumekuja hapa kuhudhuria kongamano na sio mikutano ya kiitifaki. Tumekuja kuhudhuria kongamano la kumaliza vita nchini Syria na kuzuia umwagikaji damu na ugaidi." Amesema Mikadad.
Marekani yaanza kuwasaidia waasi
Wakati hayo yakiripotiwa, Marekani nayo imeanza kutoa msaada usio wa kijeshi kwa waasi wa Syria, zaidi ya mwezi mmoja baada ya wanamgambo wenye mafungamano na al-Qaida kuteka maghala na kuchochea kukatwa kwa ghafla kwa misaada ya mataifa ya Magharibi kwa waasi.
Maafisa wa serikali ya Marekani wamesema kwamba vifaa vya mawasiliano na vitu vyengine vimeanza kutumwa kwa makundi ya upinzani yasiyo na silaha.
Ingawa msaada huo hauwezi kuwasaidia waasi kupambana na serikali wala wanamgambo wa kundi la Taifa la Kiislamu la Iraq na Sham, lakini wachambuzi wa mambo wanasema ni kama zawadi ya Marekani kwa upinzani wa Syria, baada ya kukubali kwao kushiriki mazungumzo ya Geneva.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman