Mazungumzo ya amani ya Ethiopia yaongezwa muda
10 Novemba 2022Afisa mmoja aliye karibu na duru ya mazungumzo amethibitisha zoezi hilo kuendelea hadi leo Alhamisi. Afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema mazungumzo yaliyoanza siku ya Jumatatu nchini Kenya yalitarajiwa kukamilika jana Jumatano. Mazungumzo hayo yalioongozwa na Umoja wa Afrika, yanafuatia utiaji saini wa makubaliano ya kusitisha uhasama uliosababisha mauaji ya maelfu ya watu.
Moja ya matakwa ya makubaliano hayo ni kupokonywa silaha kwa wapiganaji wa Tigray ndani ya wiki kadhaa, lakini kuna wasiwasi iwapo upande mwengine katika mgogoro huo Eritrea ambao haukuhusihswa katika mazungumzo utaweza kweli kuondoka katika eneo la mapambano la Tigray.
Duru mpya ya mazungumzo kati ya Ethiopia ya Tigray yaanza
Mambo mengine yaliyojadiliwa ni kurejesha huduma muhimu ya Intaneti, mawasiliano na huduma za benki pamoja na kufikishwa kwa misaada ya kiutu katika eneo hilo lililo na watu zaidi ya milioni 5. Hapo jana Umoja wa Mataifa ulisema bado unasubiri kupata ridhaa ya kuingia katika mkoa wa Tigray ambako hakuna kabisa vifaa vya matibabu pamoja na chakula.
Mkuu wa shirika la Afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, anaeotokea Tigray, alitarajia mpango wa utoaji wa msaada kuanza haraka baada ya makubaliano kutiwa saini wiki iliyopita.
"Hakuna kitu kinachoendelea, nikizungumzia msaada wa chakula au hata madawa, watu wengi wanakufa kutokana na magonjwa yanayoweza kutibika, wengi wanakufa kutokana na njaa. Kile tunachoamini ni kwamba hata katikati ya mgogoro raia wanahitaji chakula, na dawa hilo haliwezi kuwa na masharti." alisema Ghebreyesus.
Msaada huo huenda ukaruhusiwa ndani ya siku chache zijazo
Hata hivyo Mshauri wa Waziri Mkuu wa Ethiopia kuhusu Usalama wa kitaifa na pia kiongozi wa Ujumbe wa serikali katika mazungumzo hayo Redwan Hussein amesema huenda mwishoni mwa wiki hii au katikati ya wiki Ijayo msaada huo utaruhusiwa kuingia Tigray.
Mkuu wa idara ya dharura ya WHO duniani Michael Ryan amesema ni muhimu kwa njia ya kupitishia misaada katika maeneo ya migogoro kubakia wazi muda wote akisema kwamba watu wa Tigray wanahitaji msaada mkubwa kwa sasa na sio tu chakula na dawa lakini pia uwepo wa uhuru wa watu wa kutoa misaada hiyo ili waendelee na operesheni zao bila vizuizi.
soma zaidi: Ethiopia na Tigray wakubaliana kusitisha moja kwa moja mapigano
Vita kati ya vikosi vya serikali na vile vya waasi wa Tigray vimesababisha mgogoro mkubwa wa kibinaadamu Kaskazini mwa Ethiopia.
Kando na hilo wachunguzi wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa walisema, serikali ya Ethiopia ilitumia mbinu ya kuwanyima watu wa wa Tigray chakula kama silaha ya vita katika jimbo hilo katika mgogoro unaodaiwa kusababisha mateso makubwa kwa raia yanayoaminika kufanywa na pande zote mbili.
Chanzo: ap/afp