1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani Syria kuanza Januari 25

27 Desemba 2015

Umoja wa Mataifa unatarajia kuandaa mazungumzo ya amani baina ya serikali ya Syria na waasi yatakayofanyika tarehe 25 Januari kwa lengo la kukomesha vita vya miaka minne sasa, ambavyo vimeuwa watu zaidi ya 250,000.

https://p.dw.com/p/1HU7p
Staffan de Mistura, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria
Staffan de Mistura, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu SyriaPicha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Staffan de Mistura, imesema matarajio yao ni kwamba makundi yote ya wapinzani yatashiriki katika mazungumzo hayo yatakayofanyika mjini Geneva. ''[Staffan de Mistura] anategemea ushirikiano kamili wa wadai wote katika mzozo wa Syria, ili kufanikisha mchakato huo'', ilisema taarifa hiyo iliyotolewa Jumamosi (26 Disemba).

Mazungumzo hayo yatakuwa hatua ya kwanza ya mpango wa miezi 18 ulioidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika juhudi za kuvimaliza vita vya Syria ambavyo vimewauwa watu zaidi ya 250,000.

Changamoto ya kifo cha kamanda wa waasi

Hata hivyo, mchakato huo unakabiliwa na changamoto kufuatia kuuawa kwa kamanda wa kikundi cha upinzani kijulikanacho kama Jaish al-Islam, Zahran Alloush. Kamanda huyo aliuawa katika shambulizi la anga la jeshi la serikali, ambalo liliulenga mkutano wa siri wa viongozi wa kikundi hicho. Baadaye ilithibitishwa kuwa Alloush mwenye umri wa miaka 44 alikuwa miongoni mwa waliouawa.

Zahran Alloush, Kamanda wa waasi aliyeuawa
Zahran Alloush, Kamanda wa waasi aliyeuawaPicha: Getty Images/AFP/A.AlmohibanyGetty Images/AFP/A.Almohibany

Jaish al-Islam, kikundi kinachoungwa mkono na Saudi Arabia, ni miongoni mwa makundi ya wasi yaliyoshiriki katika mkutano wa mwanzoni mwa mwezi huu wa Desemba mjini Riyadh, na kuridhia mazungumzo na serikali ya Rais Bashar al-Assad. Wachambuzi mbali mbali wamemwelezea kamanda huyo aliyeuawa kama mtu aliyekuwa na uwezo wa kuyaleta pamoja makundi ya upinzani, wakionya kifo chake kinaacha pengo kubwa katika makundi hayo.

Kifo cha Zahran Alloush pia kimekwaza shughuli ya kuwahamisha watu 4,000 wengi wao wakiwa wapiganaji wa jihadi kutoka wilaya iliyo Kusini mwa mji mkuu wa Syria, Damascus. Shughuli hiyo, kwa mujibu wa maafisa wa serikali, ililenga kuwahamisha wapiganaji hao kutoka Qadam, Hajar al-Aswad na kambi ya ya wakimbizi wa kipalestina iliyozingirwa ya Yarmuk, na kuwahamishia katika maeneo ya Kaskazini.

Chanzo cha habari kilicho karibu na taasisi za usalama kimesema zoezi la kuwahamisha wapiganaji hao limesitishwa, kwa sababu Jaish al-Islam ilikuwa na na jukumu la kuhakikisha usalama wa mabasi yanayowasafirisha kupitia Mashariki mwa Damascus kuelekea Raqa, ziliko ngome za kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS). Wengi wa wanajihadi hao ambao wangehamishwa, ni wanachama wa IS na washirika wao wa al-Nusra Front.

'Kejeli kwa mchakato wa amani'

Mwanachama wa ngazi ya juu wa kundi la waasi linaloungwa mkono na nchi za Magharibi la Syria National Coalition, Anas al-Abdeh amesema kuuawa kwa kamanda Alloush ni 'kejeli' kwa mpango wowote wa kutafuta suluhisho la kisiasa kuhusu mzozo wa Syria, na kuongeza kuwa kimeuhujumu mpango huo hata kabla ya kuanza.

Vita vya Syria vimeuwa watu zaidi ya 250,000 na kuharibu miundombinu
Vita vya Syria vimeuwa watu zaidi ya 250,000 na kuharibu miundombinuPicha: picture-alliance/dpa/Y. Badawi

Makundi mengine mengi ya waasi vile vile yameomboleza kifo cha Zahran Alloush, yakiushutumu utawala wa rais Assad na washirika wake, hasa Urusi, kuwa na njama ya kuyadhoofisha makundi ya upinzani kabla ya kuanza kwa mazungumzo.

Mwanachama muhimu wa kundi la Ahrar al-Sham amesema makundi ya wapinzani yanapaswa kufahamu kwamba yanakabiliwa na mpango wa maangamizi, unaoendeshwa na rais wa Urusi Vladimir Putin. Kujiingiza kwa Urusi kijeshi ndani ya Syria kumelipa nguvu jeshi la serikali ya Bashar al-Assad, kwa kuwauwa makamanda wengi wa waasi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef