Syria iko tayari kushiriki mazungumzo ya amani
24 Desemba 2015Kauli hiyo ya serikali inakuja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Ijumaa iliopita kuidhinisha kwa kauli moja azimio la mpango wa amani wa kimataifa ambao utatumika katika mchakato wa amani nchini Syria.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing China Alhamisi (24.12.2015) ambao pia umehudhuriwa na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa China Wang Yi,waziri wa mambo ya nje wa Syria Walid al-Moalem amesema amemjulisha mwenyeji wake huyo kwamba Syria iko tayari kushiriki katika mazungumzo baina ya Wasyria mjini Geneva bila ya uingiliaji kati wa kigeni na kwamba ujumbe wao utakuwa tayari mara tu watakapopata orodha ya ujumbe wa upinzani katika mazungumzo hayo.
Moalem amesema "Tunataraji mazungumzo haya yatakuwa na mafanikio kuweza kutusaidia kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.Na serikali hii itakuwa na kamati ya katiba itakayokuwa na majukumu ya kuunda katiba mpya na sheria mpya ya uchaguzi ili kwamba ufanyike uchaguzi wa bunge katika kipindi cha kama miezi 18 hivi."
Serikali ya umoja wa kitaifa
Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Ijumaa iliopita lililotowa baraka zake kwa mpango wa Umoja wa Mataifa uliofikiwa katika mazungumzo yaliofanyika awali huko Vienna ambao unatowa wito wa kusitishwa kwa mapigano nchini Syria,kuwepo kwa mazungungumzo kati ya serikali na upinzani na kutowa muda wa miaka miwili kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na kuitisha uchaguzi.
Lakini vikwazo vya kukomesha vita hivyo vinaendelea kuwa vigumu huku pande zote mbili katika mzozo huo zikishindwa kujipatia ushindi wa kijeshi katika mzozo huo uliogharimu maisha ya zaidi ya watu robo milioni.
Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi mwishoni mwa juma amezikaribisha serikali ya Syria na viongozi wa upinzani kwenda China wakati serikali ya nchi yake ikiangalia njia za kusaidia mchakato wa amani wa Syria.
Baada ya kukutana na waziri mwenzake wa Syria Yang amesema mustakbali wa Syria unapaswa kuamuliwa na wananchi wake wenyewe.
Mustakbali wa Syria
Amesema "Mustakbali wa Syria na mfumo wa taifa wa Syria akiwemo kiongozi wake vinapaswa kuchaguliwa na kuamuliwa na wananchi wa Syria.Msimamo huo unakwenda sambamba na malengo na kanuni za katiba ya Umoja wa Mataifa ziada ya Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 2254 lililopitishwa hivi karibuni."
Licha ya makubaliano yao katika Umoja wa Mataifa mataifa makubwa yamegawika vibaya juu ya suala la nani wa kuwakilisha upinzani na hatima ya Rais Bashar al- Assad.
Umoja wa Mataifa unapanga kuanza mazungumzo hayo ya amani mjini Geneva mwishoni mwa mwezi wa Januari. Hiyo itakuwa duru ya tatu ya mazungumzo mjini Geneva ambapo kikao cha mwisho kilichofanyika mapema mwaka 2014 kilishindwa kuzaa matunda.
Mwandishi : Mohamed Dahman/ Reuters/AFP
Mhariri : Iddi Ssessanga