Mawaziri wa mambo ya nje wa Uganda na Rwanda wakutana Kigali
16 Septemba 2019Makubaliano ya kutatua mzozo baina ya nchi hizo yalisainiwa mjini Luanda nchini Angola na Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda.
Kwenye kikao hicho cha faragha walikuwepo pia mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, nchi ambazo ni wapatanishi kwenye mzozo huo baina ya Rwanda na Uganda.
Akifungua kikao hicho naibu waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda Balozi Olivier Nduhungirehe amesema hii ni hatua muhimu na ya kupongezwa na pande zote huku akiwashukuru mawaziri wa mashauri ya kigeni Manuel Domingos Augusto wa Angola na naibu waziri mkuu wa DRC akiwemo pia waziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi hiyo Gilbert Malamba ambao wamejitolea muda wao kwenda Kigali.
Amesema mkataba huu utakuwa na maana endapo pande mbili zitakuwa wazi na kutekeleza maazimio yake kama ilivyosainiwa na marais wa nchi hizo tarehe 21 mwezi uliopita mjini Luanda nchini Angola.
Ujumbe wa Uganda uliongozwa na waziri wa mashauri ya kigeni wa nchi hiyo Sam Kauteesa ambaye amefafanua kwamba wananchi wa Uganda na Rwanda kihistoria wamekuwa ni kitu kimoja hivyo changamoto kama hizi ni kama zinadhoofisha uhusiano huo wa enzi na enzi, huku akisema Uganda inakubaliana na kila azimio lililopo kwenye mkataba huo na kwamba iko tayari kutekeleza kila azimio kama lilivyo.
Eneo la mpaka laendelea kufungwa
Hata hivyo suala la mpaka wa nchi hizo umeendelea kufungwa, huku Rwanda ikiituhumu Uganda kuendelea kuwakamatwa raia wake kiholela, na baadhi yao kupakiwa na kurejeshwa rwanda kwa nguvu.
Hiki ni kikao cha kwanza kabisa kilichokuwatanisha pamoja mawaziri hao kutoka nchi hizi zinazozozana, kwa lengo la kuanza mchakato wa kuondoa changamoto zilizopo baina yao. Ni kikao cha tume ya dharura ambayo jukumu lake ni kuchimba mzizi wa tatizo na kuhakikisha utekelezwaji wa maazimio ya mkataba wa Angola bila masharti mengine.
Kwenye kikao cha Angola kilichowakutanisha marais wa Uganda, Rwanda,Jamhuri ya Kimokrasia ya Kongo na Kongo Brazzaville marais hao walikubaliana, pamoja na mambo mengine kuundwe tume ya dharura itakayokutana kila mara ili kufanya tathmini ya utekelezwaji wa mkataba huo.
Makubaliano ya Angola yalizitaka pande zote kuheshimu mpaka wa kila nchi pamoja na kuzuia kukamatwa kwa raia wa nchi moja wanaovuka kwenda au kupitia kwenye nchi hiyo kwenda ktk nchi ya tatu.
Hii ilifuatia hali ya kamatakamata ya raia wa Rwanda huko nchini Uganda kwa shutuma za kufanya ujasusi kwa niaba ya serikali suala ambalo siku zote Rwanda imelikanusha na kuitaja Uganda kama inayoendesha njama za kutaka kuhatarisha usalama wa Rwanda kwa kuwapa hifadhi wanaharakati wa kundi la RNC la Kayumba Nyamwasa aliyewahi kuwa mkuu wa majeshi ya Rwanda. Kwa sasa, Nyamwasa yuko uhamishoni nchini Afrika Kusini. Kwa upande wake, Uganda pia inazikanusha tuhuma za Rwanda.
Wachambuzi wanaoufuatilia karibu mzozo baina ya nchi hizo majirani ambazo siku za nyuma zilikuwa washirika wa karibu, wanaamini kuwa licha ya makubaliano ya Angola, tofauti zilizokuwepo zinaendelea kushamiri chini kwa chini.