Mawaziri wa ASEAN wakutana huko Laos
25 Julai 2024Mawaziri hao wanaanza mazungumzo ya siku tatu yanayotarajiwa kujikita katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Myanmar, mvutano katika eneo la Bahari ya China Kusini na masuala mengineyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Laos, Saleumxay Kommasith, alipoufungua mkutano huo, amewashukuru wanachama wa ASEAN na washirika wote kwa juhudi zilizoleta mafanikio makubwa huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza kazi ya kuhamasisha amani na utulivu.
Mazungumzo mapana yatakayowajumuisha pia wanadiplomasia wa eneo hilo ambao ni pamoja na Japan, Korea Kusini, India na Australia yanatarajiwa kuangazia zaidi masuala ya kiuchumi, usalama, mazingira na nishati.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken na Wang Yi wa China wanatarajiwa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana, pembezoni mwa mkutano huo unaofanyika wakati mataifa hayo mawili yakisaka kuongeza ushawishi kwenye ukanda huo.