Mauritania yaandaa uchaguzi wa bunge na mitaa
11 Mei 2023Raia nchini Mauritania wanajiandaa kupiga kura siku ya Jumamosi katika uchaguzi wa wabunge na serikali za mitaa ambao unatarajiwa kuwa mtihani muhimu kuelekea uchaguzi wa rais mwaka ujao.
Vyama 25 vinawania kuungwa mkono na wapiga kura wapatao milioni 1.8 katika uchaguzi huo wa kwanza tangu Rais Mohamed Ould Ghazouani alipoingia madarakani mwaka 2019.
Mauritania inayotambulika kama moja ya vinara wachache wa utulivu katika ukanda wa Sahel unaokabiliwa na machafuko inatarajiwa kuwachagua wabunge 176 pamoja na mabaraza 15 ya mikoa na mabaraza 238 ya manispaa.
Duru ya pili imepangwa kufanyika Mei 27 ya kuwachagua nusu ya wabunge 176 katika Bunge la Kitaifa.
Chama pekee kilichoweza kusimamisha wagombea katika majimbo yote cha El Insaf kinapigiwa upatu kushinda na haswa katika maeneo ya vijijini.