1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Sahel yafanya luteka ya kijeshi Niger

27 Mei 2024

Mataifa matano ya Kanda ya Sahel yanafanya luteka ya kijeshi magharibi mwa Niger, ikiwa ni mara ya kwanza kwa shughuli ya aina hiyo kufanywa katika eneo linalokumbwa na machafuko ya makundi ya itikadi kali.

https://p.dw.com/p/4gJF5
Askari wa Burkina Faso na Niger
Wanajeshi wa Burkina Faso na Niger wakipokea mafunzo ya kila mwaka yanayoongozwa na Marekani kukabiliana na ugaidiPicha: Issouf Sanogo/AFP

Eneo la Sahel limegubikwa kwa miaka mingi na waasi wenye mafungamano na makundi ya Al-Qaeda na Dola la Kiislamu. Wizara ya ulinzi ya Niger imesema mataifa matano ambayo ni Burkina Faso, Mali, Chad, Niger na Togo tangu Jumatatu wiki iliyopita yamekuwa yakifanya mazoezi makubwa ya kitaifa katika kituo maalum cha mafunzo ya kijeshi mjini Tillia.

Soma pia: Burkina Faso, Mali na Niger zakamilisha mpango wa ushirikiano wao

Mazoezi hayo ni pamoja na mbinu za kivita na mipango inayolenga kuimarisha uhusiano kati ya jeshi na raia wa maeneo yanayokabiliwa na vita. Shughuli hiyo inayotarajiwa kukamilika Juni 3, inaashiria luteka ya kwanza ya kijeshi ya pamoja kati ya nchi hizo tano.

Tawala za kijeshi nchini Burkina Faso, Niger na Mali ziliwafukuza wanajeshi wa Ufaransa, mtawala wa zamani wa kikoloni, na zinaigeukia Urusi kwa msaada. Nchi hizo zilifikia mkataba wa ulinzi, unaofahamika kama Muungano wa Mataifa ya Sahel, na mwezi Februari zikatangaza kujiondoa katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi - ECOWAS.