Masharti ya kudhibiti COVID yazusha maandamano ulimwenguni
21 Novemba 2021Maelfu ya waandamanaji walijitokeza katika miji mbalimbali barani Ulaya na Australia siku ya Jumamosi kupinga vikwazo vipya ambavyo vimewekwa kudhibiti virusi vya corona.
Katika siku za hivi karibuni, nchi kadhaa zimetangaza masharti makali yanayolenga kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya corona kuongezeka.
Mataifa mengine barani Ulaya yameamua kuweka vikwazo ambavyo havina athari kubwa, kama vile kuwapiga marufuku wale ambao hajapata chanjo kuingia katika migahawa au mabaa.
Soma: COVID: Ujerumani yakumbwa na ‘hali ya dharura’
Austria
Mnamo siku ya Ijumaa, Austria ilitangaza kufunga baadhi ya shughuli na biashara nchini kote, hiyo ikiwa hatua kali kuwahi kuchukuliwa na taifa lolote la magharibi mwa Ulaya katika miezi mingi iliyopita. Hatua ambayo ilisababisha maelfu ya watu kuandamana mjini Vienna.
Inakadiriwa kwamba takriban waandamanaji 35,000, wengi wakitoka katika makundi yenye misimamo mikali waliandamana Vienna. Mifano ya makundi yaliyoshiriki ni Freedom Party, wapinzani wa chanjo MFG na wale wanaojiita Identitarians.
Polisi ilisema takriban maafisa wake 1,300 walikuwa wakishika doria na waandamanaji kadhaa walikamatwa, lakini haikutoa idadi kamili.
Kuanzia Jumattau, raia milioni 8.9 wa Austria hawataruhusiwa kutoka majumbani ila tu kwa wanaokwenda kazini, dukani au mazoezini. Vikwazo hivyo vitadumu kwa siku 20 lakini vitafanyiwa tathmini baada ya siku 10.
Serikali ya nchi hiyo imetangaza kwamba itakuwa lazima kwa kila mtu kupewa chanjo kuanzia Februari 1 mwaka ujao.
Uholanzi
Nchini Uholanzi, waandamanaji walijitokeza mitaani huku wakitupa mawe Pamoja na fashifashi dhidi ya polisi, huku maandamano hayo yakigeuka kuwa ya vurugu kwa usiku wa pili mtawalia. Polisi walimtia nguvuni mtu mmoja kwenye maandamano hayo ya kupinga masharti mapya dhidi ya COVID yaliyofanyika mjini The Hague.
Siku moja kabla, watu wawili walijeruhiwa baada ya polisi kukabiliana na waandamanaji hao. Waandamanaji 51 walikamatwa kwenye maandamano yaliyofanyika mjini Rotterdam.
Mnamo siku ya Jumamosi, maelfu ya waandamanaji waliandamana katika mji wa Amsterdam.
Katika mji wa kusini mwa nchi hiyo Breda karibu na mpaka wao na Ubelgiji takriban waandamanaji mia oja walishiriki maandamano yaliyoitishwa na maDJ kupinga hatua ya kufunga mabaa, migahawa na vilabu kuanzia saa mbili usiku.
Uholanzi ilitangaza kuanza kufunga baadhi ya biashara kuanzia Jumamosi kwa muda wa wiki tatu. Kwa sasa nchi hiyo inalenga kuwapiga marufuku watu ambao hawajapata chanjo kuingia katika baadhi ya kumbi na maeneo ya umma.
Ireland Kaskazini
Katika Ireland ya Kaskazini, mamia kadhaa ya watu wanaopinga kile kinachoitwa pasipoti ya chanjo (cheti kinachoonyesha kuwa umechanjwa) waliandamana katika mji wa Belfast.
Baadhi ya waandamanaji walibeba mabango ambayo yamekosolewa pakubwa kukosa heshima, kulinganisha mikakati inayowekwa kudhibiti virusi vya corona na hatua za iliyokuwa utawala wa zamani wa kinazi nchini Ujerumani
Serikali ya Ireland Kaskazini ilipitisha kwa njia ya kura wiki hii masharti kwamba watu waonyeshe vyeti vyao vya chanjo ndipo waruhusiwe kwenye vilabu vya burudani, mabaa na migahawa kuanzia Disemba 13.
Soma: Wimbi la nne la COVID latishia vizuizi vipya Ujerumani
Croatia
Nchini Croatia, maelfu ya watu wameandamana katika mji mkuu Zagreb. Wengine walibeba bendera, ishara za kidini na mabango ya kupinga chanjo na kupaza sauti dhidi ya kile walichoelezea kuwa masharti dhidi ya haki na uhuru wa watu.
Italia
Nchini Italia, waandamanaji 3,000 walijitokeza katika mji mkuu Rome kupinga masharti kwamba wawe na pasi ya kuthibitisha kuwa wamepata chanjo ‘Green Pass', katika maeneo ya kazi, migahawa, kumbi za sinema, michezo na maeneo ya mazoezi vilevile kwenye mabasi, treni na feri.
Australia
Katika mji wa Sydney Australia, waandamanaji 10,000 walijitokeza saw ana katika miji mingine wakipinga masharti ya serikali kuwataka baadhi ya wafanyakazi kuchanjwa.
Soma: Idadi ya vifo vya corona kuongezeka barani Ulaya
Denmark na Ufaransa ni miongoni mwa nchi nyingine ambazo maandamano yalishuhudiwa katika miji yao kupinga kanuni mpya zinazowekwa ili kukabili COVID-19.