1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Mashambulizi yaendelea kuitikisa Gaza

Angela Mdungu
23 Agosti 2024

Wakati wasuluhishi wa mzozo kati ya Israel na kundi la Hamas wakiendelea na juhudi za kutafuta makubaliano ya kusitisha vita huko Qatar na Misri, mapigano yameendelea katikati mwa Ukanda wa Gaza siku ya Ijumaa.

https://p.dw.com/p/4jpMn
Khan Younis, Ukanda wa Gaza
Sehemu ya mji wa Khan Younis inavyoonekana baada ya mashambulizi ya IsraelPicha: Rizek Abdeljawad/Xinhua/IMAGO

Milio ya silaha nzito na bunduki imesikika mapema Ijumaa karibu na mashariki mwa mji wa Deir al-Balah. Kulingana na msemaji wa ulinzi na haki za jamii wa Palestina, Mahmoud Bassal,  watu wanne wameuwawa kusini mwa Khan Younis. Bassal aliripoti pia Alhamisi jioni kuwa watu 24 waliuwawa siku moja kabla kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la Israel kwenye maeneo kadhaa ya Ukanda wa Gaza.

Kwa upande wake jeshi la Israel limesema, liliwauwa wanamgambo kadhaa katika mapigano yaliyotokea Ijumaa katikati na kusini mwa Ukanda huo. Limesema, mapigano katika eneo la Khan Younis yalijumuisha mashambulizi dhidi ya maeneo yaliyokuwa yakitumika kurusha makombora kuelekea kusini mwa Israel kwa muda wa wiki moja.

Mashambulizi hayo ya anga kulingana na jeshi hilo, yaliyalenga pia maeneo 30 kote katika Ukanda wa Gaza ikiwemo miundombinu ya kijeshi na maghala ya kuhifadhi silaha.

UN: Amri za jeshi la Israel zimewalazimisha wengi kuyahama makazi yao Gaza

Katika hatua nyingine Afisa wa ngazi ya juu ya ofisi ya masuala ya kiutu ya Umoja wa Mataifa kwa Palestina  Muhannad Hadi amesema amri za kuwataka wakaazi wa Gaza waondoke katika maeneo yao  zimewakosesha makazi zaidi ya asilimia 90 ya watu milioni 2.1 wanaoishi kwenye Ukanda huo, tangu vita vilipoanza mwezi Oktoba.

Soma zaidi: Jeshi la Israel laamuru maelfu kuondoka maeneo ya Gaza

Hadi ameongeza kuwa, amri hizo zinahatarisha maisha ya raia na kuzilazimisha familia kuhama tena na tena wakati kukiwa na mashambulizi. Amebainisha kuwa raia hao wananyimwa huduma za afya, malazi, maji na mahitaji ya kiutu.

Mashambulizi ya Israel Gaza yamesababisha wengi kukosa makazi
Wakazi wa Khan Younis wakiondoka baada ya mashambulizi ya anga kuharibu makazi yaoPicha: Hatem Khaled/REUTERS

Hayo yanajiri wakati Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ikisema kuwa, Ujumbe kutoka nchini humo umeshawasili mjini Cairo kuendelea na juhudi za kuokoa makubaliano ya kusitisha vita. Mazungumzo hayo yanasimamiwa na Marekani, Misri na Qatar. Suala kubwa katika mazungumzo hayo ni pamoja na matakwa ya Israel ya udhibiti wa kudumu njia mbili za kimkakati zilizo katika Ukanda wa Gaza.

Soma zaidi: Matumaini ya kusitisha mapigano Gaza yanafifia

Harakati hizo za kutafuta suluhisho la mzozo huo zikiendelea mamlaka za Afya za Palestina zilinaripoti kuwa idadi ya watu waliouwawa kutokana na mashambulizi ya Israel tangu vita vilipoanza Otoba 7 mwaka uliopita, sasa vimevikia zaidi ya 40,260. Takwimu za mamlaka hizo zinaeleza kuwa, hadi sasa, zaidi ya watu 93,100 wamejeruhiwa.