1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendeleza mashambulizi Khan Younis Ukanda wa Gaza

12 Agosti 2024

Vikosi vya Israel vimefanya hujuma nzito kwenye mji wa Khan Younis uliopo Ukanda wa Gaza licha ya shinikizo la kimataifa la kutaka upatikane mkataba wa kusitisha vita na kuepusha kanda nzima kutumbukia kwenye mzozo.

https://p.dw.com/p/4jOFy
Vita vya Israel na Hamas huko Gaza
Vikosi vya Israel vimeendeleza mashambulizi katika maeneo ya mji wa Khan Younis mjini GazaPicha: Rizek Abdeljawad/Xinhua/IMAGO

Maafisa wa Afya wa Kipalestina wamesema mashambulizi ya jeshi ya Israel kwenye maeneo kadhaa ya mji huo yamewaua watu wasiopungua 16 na kujeruhiwa wengine kadhaa.

Soma pia: Israel yasema Iran yaandaa mashambulizi ya kulipiza kisasi

Wakati huo huo hali ya mashaka imeongezeka miongoni mwa familia za maeneo ya Ukanda wa Gaza kufuatia amri ya Israel ya kuzitaka kuondoka kupisha operesheni yake ya kijeshi.

Hayo yanajiri katika wakati kundi la Hamas limetaka wapatanishi kuishinikiza Israel ikubali mkataba wa kusitisha vita chini ya mapendekezo yaliyotolewa na Rais Joe Biden wa Marekani.

Soma pia: Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zasema vita vya Gaza viishe

Hamas imeonesha kutokuwa na matumaini na duru nyingine ya mazungumzo iliyopangwa kufanyika siku ya Alhamisi ikisema upande wa Israel unajikokota kufikia maamuzi.