Mashambulizi ya Israel yaua watu watano Rafah
26 Aprili 2024Zaidi ya nusu ya wakaazi wapatao milioni 2.3 wa Gaza wametafuta hifadhi huko Rafah, ambapo Israel imekuwa ikifanya mashambulizi ya anga karibu kila siku, huku ikionekana kujiandaa kwa operesheni kamili ya ardhini katika eneo hilo. Israel imeegesha magari ya kivita na zana mbalimbali za kijeshi karibu na mji huo wa Rafah , hali inayozusha hofu miongoni mwa raia. Mmoja wao, Mahmoud Sobh, anasema:
" Walisema kutakuwa na operesheni ya kijeshi huko Rafah, hiyo ni habari tunayosikia, kutakuwa na mashambulizi ya makombora huko Rafah. Basi tukasema tuhamie hapa Deir al-Balah, ambapo patakuwa salama. Nimekuja na binti zangu na vitu vyangu na kuja hapa Deir al-Balah na nikaweka hema langu, nina matumaini patakuwa mahali salama kama wanavyosema."
Mbali na vifo hivyo huko Rafah, watu wengine wanne wameuawa kutokana na mashambulizi ya Israel katikati mwa Ukanda wa Gaza. Wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas imesema tangu kuanza kwa mzozo huu, zaidi ya watu 34,000 wameshauawa, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.
Soma pia: Watu 22 wauawa kutokana na shambulizi la Israel mjini Rafah
Wakati huo huo, afisa mmoja mwandamizi wa Hamas ameliambia shirika la habari la The Associated Press kwamba kundi hilo, ambalo Ujerumani, Umoja wa Ulaya, Marekani na nchi nyingine zimeliorodhesha kama la kigaidi, liko tayari kufikia makubaliano ya usitishwaji mapigano kwa muda wa miaka mitano au zaidi na Israel, lakini afisa mwengine wa Hamas akasema kundi hilo litaweka chini silaha ikiwa tu kutatekelezwa suluhisho la mataifa mawili.
Hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya huko Gaza
Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema mwaka uliopita, watu walikabiliwa na viwango vilivyokithiri vya njaa huko Gaza, hali ambayo imekuwa ikiendelea kushuhudiwa kulingana na mashirika ya misaada.
Naibu mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP, Carl Skau, amesema eneo la kaskazini mwa Gaza linaelekea kukabiliwa na janga la baa la njaa kwa sababu Israel haijaruhusu usambazaji wa kila siku wa chakula kwa mamia ya maelfu ya watu wenye uhitaji mkubwa.
Skau amesisitiza kuwa tangu Israel iahidi mnamo Aprili 5 kuharakisha utoaji wa misaada, ni maendeleo kidogo tu ndio yaliyopatikana kwa sababu kiwango kinachoruhusiwa hakitoshi kukidhi mahitaji ya watu wa Gaza.
Soma pia: Watu milioni 282 duniani walikumbwa na njaa kali mwaka 2023
Katika hatua nyingine, kundi la Hezbollah limemuua raia mmoja baada ya kufanya mashambulizi ya kuvizia na kuulenga msafara wa jeshi la Israel katika eneo la mpakani linalozozaniwa kati ya Israel na Lebanon.
Pia, meli iliyokuwa ikisafiri katika Ghuba ya Aden ilishambuliwa jana Alhamisi na waasi wa Kihouthi wa nchini Yemen katika hatua yao ya kudhihirisha uungwaji mkono kwa kundi la Hamas. Makundi ya Hezbollah na Houthi yote yanafadhiliwa na Iran ambayo ni adui mkubwa wa Israel.
(Vyanzo: Mashirika)