1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasema itaijibu Urusi iwapo itaivamia Ukraine

3 Januari 2022

Rais wa Marekani Joe Biden amezungumza na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy juu ya mkusanyiko wa wanajeshi wa Urusi karibu na mpaka wake.

https://p.dw.com/p/455Qb
Kombobild Putin, Selenskyj & Biden
Picha: AFP

Wito wa Biden na Rais Volodymyr Zelenskyy umekuja katika wakati ambapo Marekani na washirika wake wa Magharibi wanajiandaa kwa mfululizo wa mikutano ya kidiplomasia ili kujaribu kukuutafutia ufumbuzi mzozo ambao Moscow imesema unaweza kuvunja kabisa uhusiano na Washington.

"Rais Biden ameweka wazi kuwa Marekani na washirika wake watajibu kwa uthabiti ikiwa Urusi itaivamia zaidi Ukraine," katibu wa habari wa Ikulu ya White House Jen Psaki amesema katika taarifa yake.

Soma piaPutin, Biden wazungumzia mzozo wa Ukraine:

Vitisho vya Urusi dhidi ya nchi za Magharibi

Psaki ameongeza kuwa Biden amesisitiza kujitolea kwake kwa kuzingatia kanuni ya "hakuna chochote kinachoweza kutendeka bila mhusika", na kwamba hawezi kujadili sera inayoweza kuwa na athari kwa bara la Ulaya bila maoni ya washirika wake.

Biden amezungumza kuhusu kuiwekea Urusi vikwazo vya kiuchumi ikiwa itavamia eneo la Ukraine, lakini amesema mwezi uliopita kwamba Marekani haina mpango wa kuchukua hatua za kijeshi.

Kremlin imedai kwamba upanuzi wowote wa NATO unatakiwa kuzitenga Ukraine na nchi zingine za zamani za KiSoviet. Warusi wamehimiza pia muungano huo wa kijeshi uondoe silaha za kujihami katika nchi za ukanda huo.

''Tunashukuru kwa msaada wa uhakika''

Marekani imepata mafanikio kidogo katika juhudi za kumshawishi rais Putin wa Urusi
Marekani imepata mafanikio kidogo katika juhudi za kumshawishi rais Putin wa UrusiPicha: AP

Marekani imetupilia mbali matakwa ya Urusi. Kanuni muhimu ya muungano wa NATO ni kwamba uanachama upo wazi kwa nchi yoyote yenye kutimiza vigezo. Na hakuna nchi isiyo mwanachama yenye kura ya turufu. Licha ya matarajio madogo kwamba Ukraine itajumuishwa katika muungano huo hivi karibuni, Marekani na washirika wake hawataki kuuondoa uwezekano huo.

Zelenskyy amesema katika ukurasa wake wa Twitter baada ya mawasiliano ya Jumapili kwamba " kudumisha amani barani Ulaya, kuzuia kuongezeka kwa vurugu na mageuzi, ndivyo vilivyojadiliwa. "Tunashukuru kwa msaada wa uhakika" Zelenskyy amesema.

Marekani imepata mafaanikio kidogo katika juhudi za kumshawishi Rais wa Urusi Vladimir Putin kulegeza mvutano. Mjumbe Mwandamizi wa Marekani na Maafisa wa Urusi wamepanga kukutana Januari 9-10 huko Geneva ili kujadili hali hiyo. Mazungumzo hayo yatafuatiwa na mikutano katika Baraza la NATO-Russia, na katika Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya.

Soma pia:EU: Yarejesha vikwazo kwa Urusi kwa kuichokoza Ukraine

Vikwazo dhidi ya Urusi

Biden alizungumza na Putin kwa takriban saa moja siku ya Alhamisi na aliwaambia waandishi wa habari siku iliyofuata kwamba alimuonya Putin kuwa uchumi wake ungepitia wakati mgumu ikiwa Urusi, ambayo imekusanya wanajeshi laki moja karibu na mpaka, ingelichukua hatua zaidi dhidi ya Ukraine.

Putin pia ameonya kwamba vikwazo zaidi dhidi ya Urusi vitakuwa "kosa kubwa." Hadi sasa pande zote mbili zimekubali kuendelea kufuata njia za kidiplomasia katika mzozo huo.