1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, Umoja wa Mataifa wahofia mauaji ya maangamizi Aleppo

Admin.WagnerD27 Julai 2012

Umoja wa Mataifa na Marekani zinasema zinahofia utawala wa Rais Bashar al-Assad unapanga mauaji ya maangamizi katika mji wa kaskazini mwa Syria wa Aleppo wakati vikosi zaidi vya serikali vikitaka kuukomboa mji huo.

https://p.dw.com/p/15fFq
Kamishna wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa.
Kamishna wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa.Picha: Reuters

Taarifa kutoka mji huo mkuu wa kibiashara wa Syria zinaelezea mashambulizi ya angani na ardhini kutoka kwa wanajeshi wa serikali, huku waasi wakielekeza mashambulizi yao kwenye vizuizi vya barabarani na vifaa vya vikosi vya usalama. Pande zote mbili zinatajwa kuepuka kukabiliana uso kwa uso kwenye uwanja wa vita katika mji huo wenye wakaazi milioni 2.5.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, amezitaka pande zote mbili kutokuwadhuru raia, huku akizungumzia wasiwasi wa Kamisheni yake dhidi ya mapambano makali ya silaha kwenye mji huo.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva, Pillay amesema kumezuka muendelezo wa vikosi vya Assad kujaribu kuushambulia mji wa Aleppo kutokea angani, ardhini na hadi msako wa nyumba kwa nyumba, katika jitihada ya kuwamaliza kabisa waasi kwenye jimbo hilo.

Wasiwasi wa mauaji ya maangamizi

Pillay ametaja kuwepo kwa ripoti zisizothibitishwa za mateso na ukatili, ikiwemo watunguaji wanaowalenga raia katika mapigano yaliyotokea hivi karibuni kwenye mji mkuu, Damascus. Ameonya kuwa wale wote wanaofanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu hawataweza kuepuka mkono wa sheria.

Mpiganaji wa waasi katika jimbo la Aleppo.
Mpiganaji wa waasi katika jimbo la Aleppo.Picha: picture-alliance/dpa

Kwa upande wake, wizara ya mambo ya nje ya Marekani, imesema kwamba kuna taarifa za uhakika kwamba idadi kubwa ya vifaru vya serikali ya Syria vinaelekea Aleppo. Msemaji wa wizara hiyo, Victoria Nuland, amesema utawala unajipanga kufanya mauaji ya kutisha.

"Hili ni jambo linalotia wasiwasi, kwamba tutashuhudia mauaji ya maangamizi kwenye mji wa Aleppo, na hilo ndilo linaloonekana kuwa serikali inapanga kulifanya." Amesema Nuland.

Mashahidi wanaelezea miripuko na milio ya risasi katika viunga vya Salahaddin, al-Sukkari na al-Fardous, huku helikopta za kijeshi aina ya MI-25 zilizotengenezwa Urusi zikilipiga eneo la al-Sakhour.

Mauaji na uasi waongezeka

Miongoni mwa watu waliouawa leo ni mzee wa miaka 60 ambaye maiti yake iliwekwa kwenye mlango wa msikiti ikisubiri kutambuliwa na jamaa zake. Hapo jana peke yake, watu 34 waliuawa huko Aleppo.

Wakimbizi wa Syria katika mpaka wa nchi hiyo na Uturuki.
Wakimbizi wa Syria katika mpaka wa nchi hiyo na Uturuki.Picha: Reuters

Katika hatua nyengine, mbunge wa jimbo hilo, amekimbilia nchini Uturuki hivi leo, akiwa mjumbe wa kwanza wa bunge ambalo linalatajwa kuwa kama muhuri kwa utawala wa Assad, kufanya hivyo.

Mbunge huyo, Ikhlas al-Badawi, amekiambia amekiambia kituo cha habari cha Sky kwamba amevuuka mpaka kuingia Uturuki na kuuacha mkono utawala aliouita wa kikatili.

Naye Brigedia Jenerali Manaf Tlas, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu na mtu wa karibu sana wa Assad aliyeasi hivi karibuni, ametangaza rasmi kujiunga na upinzani na kwamba atatumia uwezo wake kuwaunganisha wapinzani walio ndani na nje ya Syria.

Tlas alikuwa Uturuki hapo jana kwa mazungumzo na waziri wa mambo ya nje ya nchi hiyo, Ahmet Davotuglu na anatarajiwa kutembelea pia Saudi Arabia.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman