Marekani, Uingereza kusaidia dhidi ya Ebola
9 Septemba 2014Uamuzi wa Marekani kuingilia kati katika juhudi za kupambana na Ebola ulitangazwa na rais Barack Obama siku mbili zilizopita. Obama alisema nchi yake itasaidia katika ujenzi wa vituo vya kuwatenga watu waliopata maambukizi ya ugonjwa huo hatari ili wasiwaambukize wengine, na pia kuwahakikishia usalama wauguzi wanaohusika katika mapambano ya kuukabili ugonjwa huo. Obama ameutetea uamuzi huo akisema uko pia katika maslahi ya kitaifa ya Marekani.
''Tukichukua hatua hiyo sasa, bado itachukua miezi kabla ya kuweza kuudhibiti ugonjwa huo barani Afrika, lakini hautaweza kuingia Marekani'', alisema Obama na kuongeza kuwa wasipochukua hatua hiyo sasa, na ugonjwa huu ukasambaa kote duniani, ''upo uwezekano mkubwa kwamba utaweza kuenea kirahisi na kufika hapa Marekani''.
Huduma kwa wagonjwa waliotengwa
Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Kanali Steven Warren amesema jeshi la nchi hiyo litajenga hospitali ya muda yenye vitanda 25 katika mji mkuu wa Liberia, Monrovia, ambayo itakabidhiwa kwa serikali ya nchi hiyo. Afisa huyo amesema hata hivyo kuwa hospitali hiyo haitakuwa na watumishi wa kimarekani.
Liberia imeukaribisha msaada huo wa Marekani, na waziri wake wa habari Lewis Brown amesema ugonjwa wa ebola ni janga la kimataifa na hivyo jumuiya ya kimataifa inapaswa kuhusika katika kuukabili.
Katika hatua nyingine kama hiyo Uingereza imekubali kujenga kituo cha matibabu chenye vitanda 62 nchini Sierra Leone. Kitengo cha ushirikiano wa kimataifa cha nchi hiyo kimesema wahandisi na madaktari wa jeshi la Uingereza watahudumu katika kituo hicho wakisaidiwa na wafanyakazi wa shirika la msaada la Save the Children.
Kituo hicho kitakachojengwa na Uingereza kitakuwa na sehemu maalum ya kuwatibu wahudumu wa afya wanaohusika katika mapambano dhidi ya ebola, ambacho kitakuwa na vifaa bora na vya kisasa zaidi.
Vitanda zaidi vyahitajika
Kwa wakati huu vipo vitanda 570 tu katika nchi nne za Afrika Magharibi zilizoathiriwa zaidi na ugonjwa wa Ebola, na kwa mujibu wa shirika la afya ulimwenguni WHO, vinahitajika angalau vitanda 1000, mahitaji makubwa zaidi yakiwa nchini Liberia.
Shirika hilo limesema Liberia inakabiliwa na kitisho cha kupata maelefu ya maambukizi mapya ya Ebola mnamo wiki chache zijazo, na kutoa rai ya kutaka nchi hiyo ipatiwe usaidizi zaidi kuiwezesha kupambana na janga hilo.
Umoja wa mataifa umesema zinahitajika dla milioni 600 kuweza kukabiliana na kitisho cha Ebola, na Marekani tayari imeahidi kuchangia dola milioni 175. Utafiti uliofanywa na tume ya WHO nchini Liberia wiki chache zilizopita, ulibainisha kuwa ugonjwa wa Ebola tayari umeenea katika mikoa 14 kati ya 15 inayounda nchi hiyo.
Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/dpae
Mhariri:Adul-Rahman