Kongo yathibitisha vifo kutokana na Ebola
25 Agosti 2014Watu wawili wamefariki kutokana na ugonjwa wa Ebola kwenye eneo la Djera mtaani Boende, jimboni Eqauateur. Waziri wa kongo wa afya, Felix Kabange alyietoa taarifa hiyo amesema kwamba uchunguzi ulioendeshwa na wataalamu wa magonjwa ya kuambukiza kwenye taasisi ya utafiti, unaelezea kwamba watu hao, mmoja alikuwa na virusi vya aina ya Sudan na mwengine mchanganyiko wa virusi vya Sudan na Zaire aina mbili ya virusi vya ugonjwa wa Ebola.
“Baada ya uchunguzi wa sampuli nane kwenye idara ya utafiti wa kiganga nchini, sampuli mbili zimeonekana zina virusi vya Ebola. Kwa hiyo nimetangaza kuweko na ugonjwa wa ebola kwenye eneno la Dhjera huko Eqauateur”. Amesema waziri Kabange.
Hakuna uhusiano na mripuko wa Afrika Magharibi
Hata hivyo waziri Felix Kabange amesema ugojwa huo hauna uhusiano wowote na ule ulioko kwenye nchi za Afrika magharibi. Amesema waathiriwa wawili wa ugonjwa huo ni mwanamke mja mzito na mume wake ambao waliaminika kula nyama ya nyani wa misituni.
Alisema, “Ugonjwa huo hauna uhusiano na ule wa afrika magharibi kwa sababu hakukueko na mawasiliano ya aina yeyote ile baina ya wakaazi wa Djera na wale wan chi za afrika magharibi”
Kabange amesema ni kwa mara ya saba sasa ugonjwa wa Ebola kuzuka nchini DRC toka mwaka wa 1976,na jimbo la Equateur kaskazini magharibi mwa Kongo limeathiriwa kila mara na ugonjwa huo.Equateur inapatikana katika misitu na wakaazi wake wamezoea kula nyama ya wanyama mwitu.
Sehemu iliyoathirika yatengwa
Serikali imetangaza hatua za haraka za kupambana na ugonjwa huo, zikiwemo kutoruhusu wakaazi wa Djera kwenda nje ya kijiji chao. Pili kupelekwa kwa timu ya madakatari ili kuwahudumia wagonjwa na vile vile vifaa vya kuchunguza homa ya ebola. Waziri Kabange amesema kwamba watu 13 walifariki kutokana na homa ambayo hadi sasa haijafahamika kwenye eneo hilo la Eqauteur.
Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema halijathibitisha taarifa za serikali ya Kongo kuhusu ugonjwa wa Ebola hadi hapo matokeo rasmi ya uchunguzi wa sampuli zilizopelekwa Franceville - Gabon yatakapotolewa. Shirika la WHO lilielezea wiki iliopita kwamba watu 70 walifariki na homa ya matumbo kwenye eneo hilo la Equateur na kusema siyo ugonjwa wa Ebola.
Mwandishi: Saleh Mwanamilongo
Mhariri: Josephat Charo