Marekani na Saudia wakaribisha mazungumzo ya amani ya Sudan
6 Mei 2023Kwenye taarifa yao ya pamoja, Marekani na Saudi Arabia aidha wamezitolea mwito pande zote kwenye mzozo huo wa Sudan kushiriki kikamilifu kwenye mazungumzo hayo, ili kufungua njia ya usitishwaji wa mapigano na hatimaye kumaliza kabisa uhasama.
Majenerali wa pande zinazohasimiana walipeleka wawakilishi jana Ijumaa nchini Saudi Arabia kwa ajili ya mazungumzo hayo ambayo ni ya kwanza kuyakutanisha majeshi hasimu.
Majenerali wa pande hizo mbili zinazohasimiana walipeleka wawakilishi jana Ijumaa nchini Saudi Arabia kwa ajili ya mazungumzo hayo yanayofanyika katika mji wa Jeddah, ambayo ni ya kwanza kuyakutanisha majeshi hayo ya serikali yanayoongozwa na Jenerali Abdel-Fattah Burhan na RSF yaliyo chini ya Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo.
Soma Zaidi:Marekani yatishia vikwazo vipya nchini Sudan
Hatua hii inafuatia juhudi za Riyadh na mataifa mengine makubwa ulimwenguni za kuzishinikiza pande zinazozozana kukaa kwenye meza ya mazungumzo, hasa baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Hata hivyo haijulikani mazungumzo hayo yatachukua muda gani.
Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa kukutana wiki ijayo.
Awali, Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa limesema jana kwamba litafanya kikao maalumu Mei 11, kuzungumzia mzozo wa nchini Sudan.
Limesema kikao hicho kinafuatia ombi lililowasilishwa na Uingereza, Ujerumani, Norway na Marekani, ambalo hadi sasa limeungwa mkono na mataifa wengine 52.
Kulingana na msemaji wa baraza hilo jana Ijumaa, hoja kuu ya kikao hicho itakuwa ni namna mzozo huo unavyoweza kuathiri haki za binaadamu.
Soma Zaidi: Guterres: Mzozo wa Sudan sharti uzuiwe kuvuka mpaka
Mashirika ya Umoja wa Mataifa hivi karibuni yamekuwa yakiripoti visa vya mashambulizi kwenye makazi ya watu na vituo vya huduma za afya, uporaji na raia kupotezwa, vinavyofanywa na Kikosi cha Dharura, RSF.
Kulingana na Umoja huo aidha, mzozo nchini Sudan unatishia kuibua kitisho cha njaa na utapiamlo kwa watu milioni 19 katika miezi inayofuata, naibu msemaji wa katibu mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres amesema, akiunukuu mpango wa chakula duniani, WFP.
Farhan Haq amesema "WFP inakadiria kwamba idadi ya watu wasio na uhakika wa chakula nchini Sudan itaongezeka kwa kati ya watu milioni mbili na 2.5 na kufanya idadi jumla kufikia watu milioni 19 katika kipindi cha miezi mitatu hadi sita ijayo ikiwa mzozo wa sasa utaendelea."