Marekani kuendelea kuiunga mkono Ukraine dhidi ya Urusi
20 Novemba 2023Marekani tayari imetoa zaidi ya dola bilioni 40 za msaada wa kiusalama kwa Ukraine na wameahidi kuendelea kutoa msaada zaidi kadri watakavyohitajika katika kuiunga mkono Kyiv.
Washington imeihakikishia Kyiv wakati ambapo mashaka yametawala juu ya mustakabali wa msaada huo kutoka kwa wabunge wa upinzani wa chama cha Republican kwa kile walichoeleza kuwa makubaliano ya muda yaliofikiwa katika Bunge la Congress wiki iliyopita hayakuzingatia suala hilo.
Wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon imesema, ziara ya Austin ambayo haikutangazwa awali kwa sababu za usalama, imemkutanisha kiongozi huyo na viongozi wa Ukraine kuzungumzia msaada wa usalama unaohitajika kwa taifa hilo.
Waziri huyo ameahidi kuwa Marekani itaendelea kuipatia Ukraine msaada unaohitajika kadri iwezekanavyo kukabiliana na mashambulizi dhidi ya Urusi.
Hii ni ziara ya pili ya Austin nchini Ukraine tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake mnamo February 2022.
Soma pia:Urusi imefanya mashambulizi dhidi ya Ukraine baada ya wiki kadhaa ya kusimamisha mapigano
Austin amesema bila wao kuiungaji mkono Ukraine Rais wa Urusi Vladimir Putin, atafanikiwa.
Ikumbukwe kuwa mwezi Oktoba kiongozi huyo pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Antony Blinken waliwataka wabunge wao waendelee kuiunga mkono Ukraine.
Msaada wa Marekani ni endelevu kwa Ukraine
Afisa mkuu wa ulinzi wa Marekani aliwaambia waandishi wa habari kuwa msaada wa Marekani haujasitishwa na upo msaada endelevu ulioidhinishwa, na wanaamini Congress itatapitisha msaada huo.
Kwa upande wake Naibu Katibu wa Wanahabari wa Wizara ya ulinzi ya Marekani, Sabrina Singh mapema mwezi huu alisema, inawalazimu kupima kiwango cha msaada wanaotoa kufuatia upungufu wa vifurushi vya misaada ya kwenda Ukraine.
Marekani imekua ikishinikiza harakati za uungwaji mkono Kimataifa kwa Ukraine, na kuunda muungano wa kuunga mkono Kyiv na kuratibu misaada kutoka kwa mataifa kadhaa.
Soma pia:Kansela Olaf Scholz amtaka Putin kuondoa wanajeshi wake Ukraine
Wafuasi wa Ukraine wamekua wakitoa mafunzo kwa wanajeshi wa Kyiv, huku Marekani na nchi nyingine zikiiwekea Urusi vikwazo vikali, ikiwemo kwenye taasisi za fedha, masula ya teknolojia na usafirishaji wa nishati nje ya nchi.
Ziara hii ya Austin imekuja siku moja baada ya Ukraine kutangaza kuwa imevirudisha nyuma kilomita tatu hadi nane vikosi vya Urusitoka kingo za mto Dnipro, ambapo ikithibitishwa itakuwa ni hatua ya kwanza ya maana iliyofanywa na vikosi vya Kyiv kwa miezi kadhaa ya mashambulizi hayo.