1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Marekani yavitambua visiwa viwili vya Pasifiki

26 Septemba 2023

Marekani imevitambua vsiwa vya Cook na Niue kama "mataifa huru." Hatua hii inachukuliwa kama inayolenga kudhibiti kuongezeka kwa ushawishi wa China katika ukanda wa Pasifiki.

https://p.dw.com/p/4WnmO
Rais Joe Biden wa Marekani(katikati) akiwa na waziri mkuu wa visiwa vya Cook Mark Brown(kushoto) na rais wa Kiribati, Taneti Maamau(kulia) wakati wa mkutano wa mataifa wanachama wa Jukwaa la Visiwa vya Pasifiki, mjini Washington, Septemba 25,2023
Rais Joe Biden wa Marekani(katikati) akiwa na waziri mkuu wa visiwa vya Cook Mark Brown(kushoto) na rais wa Kiribati, Taneti Maamau(kulia) wakati wa mkutano wa mataifa wanachama wa Jukwaa la Visiwa vya Pasifiki, mjini Washington, Septemba 25,2023 Picha: Susan Walsh/AP/picture alliance

Rais Joe Biden amesema jana kwamba Marekani imevitambua rasmi mataifa mawili ya visiwa kwenye bahari ya Pasifiki.

Kulingana na Biden, Washington imevitambua visiwa vya Cook na Niue kama mataifa huru na kuahidi kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na visiwa hivyo.

Hatua hiyo huenda ikasaidia kuuimarisha ukanda huru na wa wazi wa bahari ya Hindi na Pasifiki, pamoja na kukabiliana na uvuvi haramu, mabadiliko ya tabianchi katika ukanda huo hatarishi, na kukuza uchumi.

Biden ameyasema hayo katika mkutano wa kilele wa siku mbili na viongozi wa wanachama 18 wa Jukwaa la Visiwa vya Pasifiki na kuwaambia serikali yake imejitoa kwa dhati kuwasaidia kukabiliana na changamoto na hasa za mabadiliko ya tabianchi.

Visiwa hivyo viwili vinakaliwa na watu karibu 20,000, lakini vinaunda eneo kubwa la kiuchumi kusini mwa bahari ya Pasifiki.