Marekani: Vikosi pinzani vimefanya uhalifu wa kivita, Sudan
7 Desemba 2023Washington aidha imedai kuwepo kwa kampeni ya safishasafisha ya kikabila katika jimbo la Darfur,
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amewasilisha ripoti hiyo iliyotokana na uchunguzi uliofanywa na wizara yake, baada ya miezi kadhaa ya kuongezeka wasiwasi na mazungumzo kushindwa kutoa suluhu.
Soma pia:Mazungumzo ya kutafuta amani ya Sudan yakwama Jeddah
Blinken amesema majeshi yote mawili ya Sudan na wanamgambo wa RSF, yamefanya uhalifu wa kivita, na kuongeza kuwa RSF pia wamefanya safishasafisa ya kikabila na uhalifu dhidi ya ubinaadamu akiangazia mauaji ya watu wengi dhidi ya jamii ya Masalit, huko Darfur.
Blinken ameyataka majeshi hayo kumaliza mzozo sasa na kuzingatia wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu, na kuwawajibisha wale wanaohusika na ukatili.
Mapigano hayo yaliyozuka katikati mwa mwezi Aprili yamesababisha watu zaidi ya milioni 6.5 kuyakimbia makazi ndani na nje ya Sudan, kusababisha vifo vya zaidi ya watu 10,000 na kudidimiza uchumi.
Soma pia:Umoja wa Ulaya wahofia kutokea mauaji mengine ya kimbari huko Darfur