Mapigano yaendelea kuutikisa mji wa Khartoum, Sudan
10 Mei 2023Hayo yanajiri huku wajumbe wa pande mbili hasimu wakiendelea na mazungumzo ya kutafuta amani nchini Saudi Arabia.
Wakaazi wameripoti mapigano makali ya ardhini katika viunga vya mji mkuu Khartoum, kati ya jeshi na wanamgambo wa kikosi cha Rapid Support (RSF).
Mapambano ya silaha nzito pia yameshuhudiwa kaskazini mwa Omdurman na mashariki mwa Bahri, miji miwili ambayo Mto Nile ndio umeitenganisha na Khartoum.
Milipuko mikubwa yaitikisa tena Khartoum
Tangu Jumanne, jeshi limekuwa likilenga maeneo ya miji mitatu, likijaribu kuwaondoa wanamgambo wa RSF ambao wamechukua udhibiti wa maeneo makubwa ya makaazi na maeneo ya kimkakati tangu machafuko hayo yalipoanza Aprili 15.
Mkaazi mmoja wa mji wa Bahri na aliyejitambulisha kama Ahmed, amesema kumekuwa pia na mashambulizi makali ya angani tangu asubuhi ya Jumatano. Ameongeza kuwa wamekuwa wakijificha kwa kulala ardhini, lakini vilevile baadhi ya watu walikimbilia mto Nile kujificha kwenye kingo zake.
Janga la kibinadamu
Machafuko hayo yamesababisha mgogoro wa kibinadamu katika taifa hilo la tatu barani Afrika kwa ukubwa, na kusababisha zaidi ya watu 700,000 kuyakimbia makwao, huku 150,000 wakikimbilia nchi jirani. Machafuko hayo pia yamesababisha ghasia katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan.
Mashambulizi yarindima Sudan, mazungumzo ya amani yakiendelea
Tayari shirika la Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa limesema hadi watu milioni 2.5 raia wa Sudan wanatarajiwa kukabiliwa na njaa katika miezi ijayo kwa sababu ya machafuko yanayoendelea.
Kulingana na shirika hilo, hali nchini humo inazidisha idadi ya wanaokabiliwa na ukosefu wa chakula kufikia milioni 19.
Mazungumzo ya Jeddah Saudi Arabia hayajazaa matundo
Lengo la mazungumzo ya Jeddah, Saudi Arabia kwa Sudan, ni kutafuta suluhisho la kumaliza vita hivyo na kuruhusu wafanyakazi wa kutoa misaada kufikisha misaada ya kiutu kwa watu wanaoathiriwa.
Makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano yamekuwa yakifeli.
Mwanadiplomasia mmoja wa nchi ya Magharibi anayefahamu jinsi mazungumzo hayo yanavyoendelea amesema, hakujakuwa na maafikiano muhimu hadi sasa, lakini wajumbe wana nia ya kuendelea na mazungumzo hadi watakapopata ufumbuzi.
Tangu machafuko hayo yalipoanza, wanamgambo wa RSF wameingia katika mitaa ya Khartoum, wameweka vizuizi kadhaa barabarani, wamechukua udhibiti wa majengo ya serikali huku walenga shabaha wao wakishika doria juu ya mapaa ya majengo.
Jeshi kwa upande wake limekuwa likifanya mashambulizi mengi ya angani kuwatimua wanamgambo hao.
(Chanzo: RTRE)