Mapigano mapya yazuka mashariki ya Congo
23 Oktoba 2023Makabiliano ya machafuko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wikendi hii yaliwahusisha waasi wa M23 dhidi ya waasi wanaoiunga mkono serikali na makundi ya waasi, na kuchochea wasiwasi katika mji wa kimkakati wa Masisi, duru kutoka eneo hilo zilisema Jumapili.
Waasi wa M23 na waasi walio tiifu kwa serikali wamekabilina katika eneo hili katika siku za hivi karibuni, wakiukiuka mkataba dhaifu wa usitishaji mapigano uliodumu kwa miezi kadhaa. "Tumejificha kanisani, waasi wa M23 wako Kitshanga tangu jana," mmoja wa wakazi alisema Jumapili.
Watu kadhaa waliojeruhiwa walipelekwa hospitali, kwa mujibu wa mfanyakazi wa afya. "Asubuhi hii, hakukuwa na wapiganaji wowote, lakini bado tunaogopa kutoka nje," duru hiyo iliongeza kusema kwa sharti ya kutotambuliwa.
"Waasi wako Kitshanga na tunajaribu kutafuta njia ya kuukomboa mji huo," duru ya usalama ililiambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, pia kwa sharti ya kutotajwa majina.
"Vita havitakoma, vitaendelea," alisema msemaji wa kundi moja la waasi linalojieleza lenyewe kama "wazalendo" wanaopambana na waasi.
Kwa mujibu wa duru ya usalama, mapigano yalikuwa yakiendelea Jumapili katika eneo jirani la Rutshuru. Kitshanga, unapatikana katika makutano ya barabara huko eneo la Masisi, kiasi kilometa 80 kaskazini magharibi ya Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.
Mji wa Kitshanga umeshuhudia mabadiliko ya mamlaka
Mara kadhaa mji wa Kitshanga umedhibitiwa na mamlaka tofauti tangu mwanzo wa mwaka huu, huku mapigano yakizuka tena wiki tatu zilizopita kufuatia mkataba dhaifu wa miezi sita wa kusitisha mapigano.
Soma pia: Congo yataka vikosi vya Afrika Mashariki viondoke
Kundi la waasi la M23 linaloongozwa na Watutsi na linaloungwa mkono na Rwanda liliudhibiti mji huo mnamo Januari, likiendeleza harakati zake za kuyateka maeneo makubwa ya ardhi. Mwanzoni mwa Oktoba, mji wa Kitshanga ulitoka mikononi mwa kikosi cha kimataifa kilichotumwa na Jumuiya ya Afrika Masahriki, ambacho kiliweka eneo ambalo halikuruhusiwa shughuli za kijeshi kati ya makundi ya waasi, na kuingia mikononi mwa waasi wa eneo hilo na kwa saa 24 ukadhibitiwa na kundi la M23, kabla waasi hao kuondoka mjini humo.
Mnamo Oktoba, jeshi, ambalo linadai kusimamia usitishaji mapigano kufuatia amri ya mpatanishi wa kikanda, lilikuwa limeandaa safari na vyombo vya habari kwenda mjini Kitshanga wiki moja kabla mji huo kuanguka tena mikononi mwa waasi.
(afp)