Congo kulegeza baadhi ya masharti ya utawala wa kijeshi
13 Oktoba 2023Katika hotuba yake kwa taifa iliyopeperushwa Alhamisi ( 13.10.2023) jioni kupitia televisheni, Rais Tshisekedi amesema kuwa amri ya kutotoka nje itaondolewa na maandamano ya amani kuruhusiwa chini ya mchakato wa kulegeza kwa utaratibu baadhi ya sheria katika mikoa iliyoathirika. Rais huyo amesema kuwa amefanya maamuzi kuhusu utekelezaji wa mpango wa mpito utakaotekelezwa kwa hatua ambao utafikisha kikomo hali ya kipekee inayoshuhudiwa kwa sasa.
Baadhi ya hatua zitakazochukuliwa
Rais Tshisekedi ameongeza kuwa , mpangilio huo wa mpito utajumuisha kuanzisha tena mamlaka ya kiraia katika taasisi za maeneo hayo zilizogatuliwa ambazo tayari ziko chini ya udhibiti wa vikosi vya kijeshi vya Kongo.
Soma pia:Tshisekedi awataka waasi kuweka chini silaha Kongo na kuweka amani
Kiongozi huyo pia amesema kwamba ataondoa vikwazo vya kikatiba na kwa mara nyingine tena kuruhusu usafiri huru wa watu na bidhaa. Hali hiyo ya kuzingirwa ambayo ni sawa na hali ya hatari, iliwekwa katika majimbo hayo mnamo mwezi Mei mwaka 2021, huku serikali ikitaja haja ya kudhibiti ghasia na kurejesha utulivu.
Mashirika ya haki za binadamu yahoji hitaji la sheria zilizoko
Mashirika ya kutetea haki za binadamu mara kwa mara yamehoji uhalali na hitaji la hatua hizo, ambazo ziliruhusu kuwekwa kizuizini kwa watu wengi kabla ya kufunguliwa mashataka na kuzuiwa kwa uhuru wa kutembea.
Soma pia:Kuna jumla ya makundi 266 yanayomiliki silaha mashariki ya Kongo
Wakati Rais Tshisekedi anapofanya kampeni za kuwania muhula wa pili, imebidi utawala wake ukanushe madai kutoka kwa makundi ya kutetea haki na washirika wa kimataifa kuhusu ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza na upinzani wa kisiasa.
Amnesty International yasema sheria zilizowekwa zilichangia kudorora kwa haki za binadamu
Mwaka jana, wataalam wa Umoja wa Mataifa na wa shirika la Amnesty International, walisema kuwa usalama ulikuwa umedorora tangu kuwekwa kwa hali ya kuzingirwa kijeshi. Amnesty iliitaka serikali ya Kongo kukomesha sera hiyo, ikisema pia ilisababisha kuzorota kwa hali ya haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kunyanyaswa kwa wanahabari na kuuawa kwa wanaharakati.
Soma pia: Makundi ya waasi yasababisha mauaji Mashariki mwa Congo
Licha ya kuwepo kwa wanajeshi wa Kongo na walinda amani wa Umoja wa Mataifa, mara kwa mara raia hukabiliwa na mashambulizi kutoka kwa mamia ya wanamgambo katika maeneo ya Kivu Kaskazini na Ituri
tangu kumalizika kwa vita vya kikanda mwaka 2003.
Watu wapatao milioni 6 walihama makazi yao
Mnamo mwezi Novemba, mwakilishi mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo alisema kuwa ukosefu huo wa usalama umesababisha watu wapatao milioni 6 kuyahama makazi yao .
Siku ya Alhamisi, ubalozi wa Marekani ulisema ulikuwa na wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ghasia katika eneo la Kivu Kaskazini. Katika taarifa, ubalozi huo umeongeza kuwa mgogoro Mashariki mwa DRC Unahitaji suluhu la kisiasa na sio la kijeshi.