1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi awataka waasi Kongo kuweka chini silaha

Jean Noël Ba-Mweze
15 Agosti 2023

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasoa ya Kongo Félix Tshisekedi ameyatolea wito makundi ya wapiganaji nchini humo kuweka chini sialha na kujiunga na mpango wa amani

https://p.dw.com/p/4VBW4
Felix Tshisekedi Präsident DR Kongo
Rais Tshisekedi atagombea uchaguzi kwa muhula wa piliPicha: Isa Terli /AA/picture alliance

Ametoa wito huo katika siku ya pili ya mkutano wa kutathmini hali ya dharura iliyotangazwa katika mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini miaka miwili iliyopita. Mashirika ya kiraia yanasema utawala wa kijeshi uliowekwa katika mikoa hiyo chini ya hali hiyo ya dharura umeshindwa kurejesha amani na usalama, na kutaka ukomeshwe.

DR Kongo Rethy | militante Milizgruppe URDPC/CODECO
Makundi ya waasi yanaendesha harakati IturiPicha: ALEXIS HUGUET/AFP

Mkutano huo ulioitishwa na serikali ya Kongo unawakutanisha hapa Kinshasa tangu jana Jumatatu, baadhi ya wanasiasa na viongozi wa kijamii pamoja na wale wa mashirika ya kiraia ili kutathmini kwa usahihi, hali ya mzingiro yaani utawala wa kijeshi huko Ituri na Kivu Kaskazini. Rais Félix Tshisekedi aliwataka washiriki kuchukua hatua zozote zinazohitajika ili kurejesha amani na usalama katika mikoa hiyo miwili. Alitoa wito kwa waasi na makundi mengine yanayomiliki  silaha kuchukua fursa ya mwisho iliyotolewa na serikali kwa ajili ya  amani.

"Siwezi kumaliza hotuba yangu bila kutoa wito wa kizalendo kwa Wakongo ambao kwa bahati mbaya bado wanafanya vitendo vya uasi dhidi ya nchi hii. Napenda kulihakikishia taifa kuwa serikali imejitolea kwa nia njema kutoa fursa ya mwisho kwa makundi ya uasi kujisalimisha kwa amani."

Mzingiro wa Ituri na Kivu ya Kaskazini

Mikoa ya Ituri na Kivu kaskazini imekuwa chini ya utawala wa kijeshi tangu Mei 6 mwaka 2021. Utawala maalum ulioamriwa na Rais Tshisekedi kwa lengo la kurejesha amani na mamlaka ya Serikali huko. Lakini wakazi wa mikoa hiyo miwili wanatarajia tu mkutano wa Kinshasa kukomesha  hali hiyo ya kuzingirwa, kama alivyoeleza Dieudonné Lossa Dekhana, mratibu wa mashirika ya kiraia mkoani Ituri.

"Hakuna hata kundi linalomiliki  silaha lililoondolewa katika eneo la Ituri. Idadi ya makundi yenye silaha imeongezeka wakati wa hali ya kuzingirwa na tumeorodhesha  watu kadhaa waliouawa na wengine kadhaa kuyahama makazi yao. Wakazi wa Ituri wanatarajia tu kukomeshwa hali ya kuzingirwa kwani haikukuwa na ufanisi."

Wahudhuriaji mkutano huo wana siku tatu za kujadili na kutoa mapendekezo. Yaani kazi ya mkutano huo inaendelea hadi kesho Jumatano