Mapigano makali yashuhudiwa Khartoum
20 Julai 2023Jeshi la Sudan limekishtumu kikosi cha RSF kwa kulenga eneo la makazi katika shambulio la ndege isiyo na rubani na kusababisha vifo vya raia 14 na na kuwajeruhi wengine 15.
Mzozo huo ulioanza Aprili 15 mwaka huu, kati mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na hasimu wake ambaye ni makamu wake wa zamani, na kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Daglo, tayari umesababisha vifo vya takribani watu 3,000 na wengine zaidi ya milioni 3.3 kuyahama makazi yao.
Vitendo vya uwagaji damu vimeripotiwa pia katika jimbo la Darfur. Wiki iliyopita, mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC Karim Khan alisema wameanzisha uchunguzi mpya kuhusu madai ya uhalifu wa kivita huko Darfur na kuonya dhidi ya "kuruhusu historia kujirudia" eneo hilo ambapo watu 300,000 waliuawa katika mzozo wa mwaka 2003 ambao ulipelekea ICC kumfungulia mashtaka ya mauaji ya halaiki kiongozi wa zamani Omar al-Bashir.