Mapigano kati ya kundi la M23 na Wazalendo yazua hofu Kongo
28 Desemba 2023Wakaazi wa mji wa Kibumba wakielezea pia kusikia milio ya risasi kwenye mji huo ambako makundi ya vijana wazalendo walikuwa wakirusha mabomu kuelekeangome za M23.
Ni wakati vikosi vya jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC vikiwasili Goma kupambana dhidi ya M23.
Waasi wa M23 wamezidisha mashambulizi yao dhidi ya vijiji vya walayani Masisi ambako hofu imetanda kwenye meneo yanayolengwa kwa makombora toka kundi hilo.
Soma pia:UN yajiandaa kuanza kuondoa walinda amani DR Kongo
Kulingana na vyanzo vya kiraia, M23 imekita ngome yake sasa kwenye milima ya kijiji cha Mitumbala nje kidogo na mji wa sake ambako mapigano makali yaliendelea hadi jana Jumatano baina yao na makundi ya wapiganaji wanaojiita wazalendo wanaoungwa mkono na jeshi la kongo.
Waasi wa M23 wanaodaiwa kupata msaada kutoka kwa Rwanda, ambayo inakanusha hilo wameelezwa pia kufika katika milima ya Kagano na Rucika inayokaribia mji wa Bweremana ambao ni muhimu kwa usambazaji wa chakula kwenda mjini Goma.
Milio ya risasi yasikika milima ya Mitumbala
Wakaazi wa Sake wamethibitisha kutekwa kwa milima ya Mitumbala ambako milio ya risasi ilirindima kwa siku tatu mfululizo wakati vijana wazalendo walipojaribu kuwafurusha M23 bila mafanikio.
Wakati huo huo, jeshi la Jamhuri ya kidemokrasia ya kongo limetumia hii leo ndege kivita kushambulia ngome za M23 kwenye milima ya karuba ambako mapigano yameendelea hadi mchana wa leo nakuongeza hofu kubwa kwa raia wanaokimbia kuelekea mji wa Madini wa Rubaya wilayani humo.
Soma pia: M23 wakamata mji mashariki mwa Kongo
Pia Ripoti zinasema kuwa, vijana wazalendo wenye silaha walikabiliana jana usiku na M23 nje kidogo na mji wa kibumba kilometa 20 kaskazini mashariki mwa mji wa Goma ambako hali ilikuwa ni ya wasiwasi mchana kutwa wa leo alhamisi.
Hapo jana Jumatano askari wa Afrika Kusini kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC waliwasili Goma wakiwa na agizo la kupambana moja kwa moja na waasi wa M23, tofauti na jeshi la kanda ya Afrika Mashariki ambalo wanajeshi wake wa mwisho waliondoka mapema mwanzoni mwa juma hili.
Kuwasili kwa wanajeshi hao wa Afrika Kusini kumethibitishwa na shirika la habari la Kongo, ASP.