Maoni: MDC imekatisha tamaa
5 Agosti 2013Ni jambo la rahisi, kuukosoa Umoja wa Afrika, ambao ni kama simba asiyekuwa na meno, kwa kupitisha matokeo ya uchaguzi ya Zimbabwe yanayosemekana kuwa si halali. Umoja wa Afrika hauko pekee yake. Hata Jumuiya ya maendeleo ya nchi Kusini mwa Afrika, SADC, inafahamika kwa kutokuwa na ukali katika maswala yahusuyo Zimbabwe. Mara ya mwisho hilo lilionekana mwezi Juni, pale ambapo Mugabe alichukulia wito wa SADC wa kutaka uchaguzi usogezwe mbele kama kuingiliwa katika siasa zake za ndani.
Lakini jambo linalosikitisha zaidi katika uchaguzi huu ni chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change MDC. Mhariri wa Gazeti la "Der Standard" la Austria, anaandika: "Nina shaka kwamba Morgan Tsvangirai angeweza kushinda uchaguzi hata kama mambo yangekwenda vizuri zaidi." Hapo amesema ukweli kabisa. Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai anaulaani udanganyifu uliofanyika wakati yeye mwenyewe amekuwa mdanganyifu dhidi ya matumaini ya mamillioni ya Wazimbabwe.
Starehe badala ya siasa
Tsvangirai ambaye awali alionekana kama mhanga wa kisiasa baada ya kupigwa na wababe wa Mugabe, katika kipindi cha kampeni alisikika zaidi kwa sababu ya kashfa za ngono na si kutokana na mipango ya kisiasa au ya kiuchumi aliyokuwa nayo kwa nchi yake. Inakuwaje Tsvangirai aonekane katika meli ya starehe karibu na Singapore wakati nchini mwake watu wanaangamia kwa njaa? Na inakuwaje akarabati nyumba aliyopewa na serikali kwa dola za Kimarekani millioni 4.5?
Zamani, wanadiplomasia waishio Zimbabwe walizungumza kwa furaha juu ya Tsvangirai. Leo hii wanakubaliana na kichwa cha habari cha gazeti la The Herald lenye mafungamano na chama tawala cha ZANU-PF, kwamba Tsvangirai alijishughulisha zaidi na wanawake badala ya kuwaza uchaguzi.
Vijana wa Afrika hawataki siasa za zamani
Vijana wa Kiafrika wameigeuzia siasa mgongo. Wamechoshwa na serikali zinazoshindwa kufanya kazi ipasavyo. Mbaya zaidi ni kwamba wanaugeuzia pia mgongo upinzani ambao ungeweza kuwa chaguo mbadala. Kuanzia Kenya hadi Angola, Ethiopia hadi Mali, upinzani unaonekana kuwa wa kifisadi na wenye uelewa finyu kama wanaotawala ikulu.
Huu ndio ukweli wa kusikitisha juu ya Zimbabwe na nchi nyingine za Kusini mwa Afrika. Haina haja ya kusifu ukuaji wa kiuchumi wa nchi za Kiafrika iwapo upinzani nao unalenga tu kupora mali za nchi. Bila kuwa na upinzani wenye mpango madhubuti na wenye viongozi wenye uadilifu, Afrika haiwezi kusimama kwa miguu yake yenyewe.
Mwandishi: Ludger Schadomsky
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman