1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko Afrika Kusini yafichua kushindwa kwa serikali

Claus Stäcker Lilian Mtono
15 Julai 2021

Afrika Kusini imetikiswa na ghasia mbaya kabisa katika miaka kadhaa, ambazo zimechochewa na kifungo cha aliyekuwa rais wa taifa hilo Jacob Zuma. Lakini kuna sababu zaidi za uporaji na fujo, anaandika Claus Stäcker.

https://p.dw.com/p/3wWEO
Südafrika - Proteste und Gewalt nach Verurteilung von Jacob Zuma
Picha: Siphiwe Sibeko/Reuters

Wakati machafuko hayo yakiendelea kutokota hata hivyo sababu hasa zilizochangia watu kupora na machafuko hayo zinakwenda mbali zaidi ya kile kinachoshuhudiwa kwa macho. 

Haihitaji kazi kubwa kuchochea machafuko ya kisiasa nchini Afrika Kusini. Nchi hiyo ina historia ndefu ya machafuko: vurugu za kisiasa, vurugu za ubaguzi wa rangi, vurugu zinazotumiwa kuanzisha mizozo ya kikabila, vurugu za kijamii na vurugu za uhalifu. Mambo hayo yote kawaida hufanya hali kuwa tete.

Kwa muda mrefu kumeshuhudiwa maandamano yaliyohusishwa na huduma mbovu, na waandamanaji walielezea ghadhabu dhidi ya utoaji mbovu wa huduma na watumishi wa umma wanaokula rushwa. Mara nyingine kuliibuka minong'ono na hotuba za chuki hatua zilizochochea machafuko ya makundi ya kihalifu na yenye silaha dhidi ya wahamiaji.

Stäcker Claus Kommentarbild App
Mkuu wa idhaa za Kiafrika wa DW, Claus Stäcker.

Lakini kifungo cha sasa cha aliyekuwa rais wa taifa hilo Jacob Zuma ndicho hasa kimechochea kile kinachoonekana nchini humo. Aliyewahi kuwa mkuu wa opereshini ya kiintelijensia enzi ya utawala wa Zuma Thulani Dlomo analaumiwa kwa kuandaa machafuko haya ya sasa, yaliyoanzia katika mkoa wa Zuma la KwaZulu Natal. 

Wakati Zuma alijisalimisha mwenyewe kwa serikali, ungeona moja kwa moja kwenye mtandao wa intanet jinsi machafuko yalivyoanza na kusambaa kote katika mkoa wake wa nyumbani wa KwaZulu-Natal hadi mkoa wa Guateng na maeneo yake ya Johannesburg na Pretoria yenye mchanganyito wa watu.

Na bado, machafuko hayo hayahusiani na Zuma, bali mfumo alioutengeneza. Chini yake, serikali imeshindwa kufanya kazi. mashirika ya upelelezi, na polisi yote yameingiliwa na wafuasi wake watiifu. Chama tawala cha ANC kimegawanyika kisiasa na kikabila, kimedhoofika na kwa sasa hakina uwezo wa kufanyiwa mageuzi.

Rais Cyril Ramaphosa amejaribu kusafisha na kuvipa majukumu vikosi maalum na mashirika ya upelelezi kufanya kazi wanayostahili kufanya. Hadi hivi karibuni, hakuna mtu ambaye angeweza kuamini kuwa Zuma angekuwa jela na kuwa baadhi ya washirika wake wa karibu wangekuwa chini ya uchunguzi wa mfumo wa sheria.

Na licha ya hayo, machafuko mabaya katika siku za karibuni yanaonesha kwamba serikali inaendelea kutofanya kazi. Pamoja na zaidi ya vifo 70 katika vurugu za sasa, kuna karibu vifo 700 na maambukizi mapya zaidi ya 12,000 kutokana na janga la Covid-19 kila siku.

Südafrikas ehemaliger Präsident Jacob Zuma
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma akiwa mahakamani, wakati alipokuwa akisikiliza madai dhidi yake.Picha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Soma Zaidi: Vurugu zaendelea Afrika Kusini baada ya kufungwa kwa Zuma

Vikosi vya usalama navyo vimeonekana kushindwa kusimamia ipasavyo vizuizi dhidi ya kusambaa kwa virusi hivyo, ikiwa ni pamoja na hatua ya kufunga shughuli nchini humo. Hali ya ustawi imekuwa duni, huku biashara muhimu ambazo serikali ina mkono wake zikiwa zimezoroteshwa na ufisadi na usimamizi mbovu. Na baada ya miezi sita ya janga la virusi vya corona uchumi wa Afrika Kusini umezorota kwa kiasi kikubwa.

Na mbaya zaidi, maduka makubwa ama supermarkets, maduka ya dawa na biashara yameporwa na hata wale walio na bishara ndogondogo nao sasa wanakosa riziki zao za kila siku. Hata sekta isiyo rasmi, wafanyabishara wadogowadogo ambao hawajasajiliwa na watoaji  huduma wadogowadogo, ambao katika nyakati za kawaida huwalisha kariban nusu ya raia wa Afrika Kusini, nako hali ni tete.

Ni wazi kuwa Ramaphosa yuko njia panda. Wawekezaji ambao amekuwa akiwavutia huenda sasa wakaondoka na kwa maana hiyo kuibuka kwa matatizo ya kiuchumi. Kuna uwezekano kwamba machafuko hayo yatakwisha haraka, lakini kutarajiwe tatizo la kutokuelewana miongoni mwa jamii litaendelea kutokota.