Vurugu na uporaji waripotiwa kabla ya rufaa ya Jacob Zuma
12 Julai 2021Shirika la upelelezi la Afrika ya kusini limesema watu 6 wameuliwa na wengine 219 wamekamatwa tangu kuanza kwa machafuko hayo. Ghasia hizo awali zilitokea katika mkoa wa Kwazulu Natal anakotokea Zuma siku ya Jumatano usiku wakati alipoanza kutumikia kifungo chake cha miezi 15 gerezani kwa kukiuka maagizo ya mahakama. Polisi inasema kuwa wahalifu wanatumia ghadhabu dhidi ya hatua hiyo kuiba na kusababisha uharibifu.
Wahusika kufunguliwa mashtaka
Akizungumza jana, rais Cyril Ramaphosa amesema ghasia zinavuruga juhudi za kuujenga uchumi wa nchi hiyo wakati ambapo kuna janga la COVID-19. Ramaphosa amesema hakuna uhalali wowote wa kufanya vurugu wala uharibifu wa mali.
''Tuwe wazi, kama taifa, kwamba hatutovumulia vitendo vyovyote vya uhalifu. Hatutovumilia vitendo vyoyote vya uharibifu. Wale waliohusika na visa hivyo vya umwagikaji wa damu watakamatwa na kufunguliwa mashtaka''
Rais Ramaphosa amesema ingawa kuna walioumizwa na wenye hasira kwa sasa, nilazima wazingatie juhudi za kupambana na janga la corona nchini humo. Kwa kipindi cha wiki mbili, Afrika ya Kusini imeshuhudia visa 20,000 kwa siku vya maambukizi ya Corona. Na watu 4,200 wamefariki mnamo kipindi hicho kutokana ugonjwa huo, alisema Ramaphosa.
Ghasia zilizuka jana Jumapili kwenye miji kadhaa ya Afrika Kusini. Mbali na jimbo la KwaZulu-Natal, vurugu hizo zilienea hadi kwenye jimbo la Gauteng na jiji la Johannesburg. Waandamanaji walipora maduka,kuchoma moto majengo na magari na vilevile kuzuia barabara wakati wakiandamana kwenye miji hiyo.
Sarafu ya Rand ya poromoka
Mjini, Eshowe, karibu na makaazi ya Nkandla ya Jacob Zuma, polisi walifyatua risasi mapema leo Jumatatu kuwatawanya waandamanaji waliopora na kuliteketeza duka kuu la mji huo. Polisi imesema malori yalichomwa moto kwenye barabara kuu karibu na mji wa bandari wa Durban.
Sarafu ya Afrika ya Kusini iliporomoka leo Jumatatu kwa asilimia moja. Wakati huohuo mahakama kuu ya nchi hiyo inatarajiwa kusikiliza leo ombi la Zuma la kutotumikia kifungo. Siku ya Ijumaa ombi lake la kutolewa gerezani lili kataliwa na korti ya mkoa.