Maoni: Hatimaye Ujerumani yaja na msimamo dhidi ya Urusi
28 Februari 2022Hotuba hii imetolewa wakati muafaka kabisa anasema Kasper-Claridge.
Hotuba hiyo kuhusu Ukraine ambayo kansela Olaf Scholz aliitoa mbele ya bunge siku ya jana, ilionekana kuwa iliyojaa mamlaka na ambayo ilikuwa na ujumbe wa wazi kwamba hatimaye ilihitimisha zile zama za kujiuliza na mashaka lakini pia siasa za kuchukua hatua kwa kujikongoja.
Ujerumani hatimaye inapeleka silaha nchini Ukraine na kuwekeza pakubwa kwenye jeshi lake. Hatua hii inaashira mwanzo wa enzi mpya na uhalisia ambao kansela mwenyewe aliurejelea mara kwa mara.
Soma Zaidi: Rais wa Ukraine atoa agizo kwa wananchi wote kufanya maandalizi ya kujihami
Serikali ya muungano ya Ujerumani imejitanabahisha kwa msimamo wa wazi dhidi ya uvamizi wa Urusi. Hatimaye washirika wa muungano wa kujihami wa NATO na hususan wa mataifa ya Baltiki sasa wanajua wanasimamia wapi na Ujerumani. Yapo mashaka kwamba Urusi inataka kuyalazimisha mataifa hayo kuingia kwenye himaya yake ya ushawishi, pamoja na Ukraine. Scholz ameweka wazi kwamba Berlin haitaendelea kulivumilia hilo na itasimamia kwa dhati wajibu wake kwa NATO.
Ama kwa hakika, huu ni wakati muafaka baada ya mrefu Ujerumani kujihuisha tu na mazungumzo na makubaliano ya kisiasa.
Hata hivyo, na hili ni msingi mno, maridhiano kati ya Urusi na Ujerumani kihistoria yanasalia kuwa nguzo muhimu ya siasa za Ujerumani, kama Scholz alivyosisitiza. Hiyo ilikuwa ni ishara muhimu kwa watu wa Urusi, ambao kwa namna yoyote ile hawaungi mkono hatua ya rais Vladimir Putin ya kuivamia Ukraine. Maandamano katika majiji kadhaa ya Urusi yanathibitisha hilo.
Itakuwa ni gharama kubwa.
Lakini tusijidanganye wenyewe, anasema Manuela Kasper-Claridge. Enzi hii mpya ya Ujerumani itakuwa ghali na pengine ya maumivu makubwa. Jeshi la Ujerumani ama Bundeswehr linajiandaa kupewa Euro bilioni 100 za ziada kwa mwaka huu tu. Urusi nayo, huenda ikatengwa katika mfumo wa kiuchumi wa dunia. Kupanda kwa bei ya mafuta, vizuizi katika usambazaji na anguko la wastani katika biashara ya malighafi ndio yanatarajiwa kuwa athari za mwanzoni kuanza kushuhudiwa.
Ujerumani itatakiwa kujiandaa yenyewe. Serikali italazimika kuchukua hatua za haraka kuonyesha namna taifa linavyotakiwa kukabiliana na hali hiyo na kuelezea matokeo yake, lakini pia mshikamano na upinzani. Kinachotakiwa hapa ni kushikana pamoja, lakini bila ya kupuuza mijadala ya ukosoaji.
Ni haki kwamba Ujerumani hatimaye inaunga mkono hatua za kuzifungia benki za Urusi katika mfumo wa kimataifa wa malipo wa SWIFT, lakini katika hili pia kuna haja ya athari hizo kuzungumziwa. Kuna uwezekano pia kwamba usambazaji wa gesi kutoka Urusi hadi Ujerumani nao ukasimama kwa sababu bila ya SWIFT haitawezekana kulipia gesi hiyo.
Soma Zaidi:Vikwazo vipya dhidi ya Urusi ni vikali kiasi gani?
Sio tu kofia ngumu, lakini pia uwazi.
Hatua hii hatimaye itawahakikishia raia wa Ukraine ya kwamba Berlin iko tayari kufanya zaidi badala tu ya kupeleka kofia ngumu 5,000. Ni ujumbe muhimu kutoka kwa kansela na serikali yake ya muungano wa Social Democrats, Kijani na Waliberali.