Manuel Noriega: Kifo cha dikteta
Askari wa zamani, raia wa Panama aliyetawala kimabavu Manuel Noriega amefariki hospitalini akiwa na miaka 83. DW inaangazia kuibuka kisiasa kwa mwanajeshi huyo aliyewahi kuwa mshirika wa Marekani pamoja na kuanguka kwake
Maisha akiwa mwanajeshi
Alizaliwa katika familia ya kimaskini mwaka 1934 katika mji wa Panama. Manuel Antonio Noriega aliingia jeshini akiwa na umri mdogo. Baada ya kupata udhamini wa kusoma katika chuo cha kijeshi cha nchini Peru, alijiunga na jeshi la taifa cha Panama na kupandishwa vyeo kwa haraka.
Jasusi wa shirika la kijasusi la Marekani, CIA
Noriega aliwahi kuhudumu kama mtoa siri wa shirika la kijasusi la Marekani, CIA kwa miaka mingi na mahusiano ya karibu na Marekani kabla ya kuchukua mamlaka Panama mwaka 1983. Alitawala kwa mabavu na kutoa amri watu kuuawa na kughushi matokeo ya chaguzi. Lakini pia alitengeneza fedha kwa biashara ya dawa za kulevya na wafanyabiashara wakubwa wa Colombia, ingawa aliendelea kufanya kazi na Marekani
Kwanza rafiki, kisha adui
Mahusiano ya Noriega na matajiri wa dawa za kulevya hatua kwa hatua yalisababisha kuvunjika kwa mahusiano na Marekani. Mwishoni mwa miaka ya 80, maafisa kutoka ndani ya serikali yake walimtuhumu kwa ufisadi na kuanzisha maandamano ya umma. Marekani iliondoa misaada kwa mshirika wake huyo wa awali na kuivamia mnamo mwaka 1989.
Hatia ya uchuuzi wa dawa za kulevya
Wanajeshi wa Marekani waliingia Panama Disemba 20 na kuviangusha vikosi vya Panama na kuchukua udhibiti. Noriega alitoroka na kwenda kujificha, na kujitokeza siku chache baadae katika ubalozi wa Vatican ulioko mjini Panama. Alijisalimisha kwa majeshi ya Marekani Januari 3, 1990, na kupelekwa Florida ambako alifungwa kwa miaka 17 kwa kosa la biashara ya dawa za kulevya na kutoa huduma bandia.
'Uso wa nanasi'
Noriega, ambaye aliitwa kwa jiina la utani "Uso wa nanasi" kutokana na uso wake kujaliwa na makovu ya chunusi, alionekana kuwa mpole alipokuwa jela. Mwaka 2015, aliomba msamaha kwa makosa ya unyanyasaji ambayo yalifanywa wakati wa utawala wake, wakati alipohojiwa na kituo cha televisheni cha Panama cha Telementro. Alisema anatamani kutamatisha mzunguko wa zama za kijeshi.
Maisha akiwa jela.
Noriega aliishi muda mwingi akiwa jela, nchini Marekani, Ufaransa na Panama kuanzia makosa ya kuuza dawa za kulevya, mauaji na huduma bandia. Picha hii ya mwaka 2011, Noriega anaonekana akiwasili katika gereza la Renacer lililoko Panama kutumikia kifungo cha miaka 20 kwa makosa ya kupotea kwa wapinzani wake wa kisiasa wakati wa utawala wake. Aliachiwa kwa muda Februari 2017 ili kufanyiwa upasuaji.