Mamilioni ya Wanigeria walala gizani kufuata mgomo wa taifa
4 Juni 2024Mgomo huo pia umesababisha safari nyingi za ndege kufutwa katika uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi wa Lagos na katika mji mkuu Abuja huku abiria wasijue la kufanya.
Muungano wa vyama vya wafanyikazi nchini Nigeria jana uliizima gridi ya taifa ya umeme na kutatiza pakubwa safari za ndege baada ya kuanza mgomo uliochochewa na hatua ya serikali kushindwa kukubaliana juu ya kiwango kipya cha mshahara wa chini.
Mgomo huo ulianza baada ya mazungumzo kuvunjika kati ya serikali na vyama viwili vikuu vya wafanyikazi – NLC na TUC juu ya kuongeza kima cha chini cha mshahara. Mgomo huo ni wa nne kufanyika katika taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika tangu Rais Bola Tinubu alipoingia madarakani mwaka uliopita.
Soma pia: Mgomo wa wafanyakazi watatiza usafiri wa ndege Nigeria
Vyama vya wafanyikazi vinashinikiza nyongeza ya kima cha chini cha mshahara kwa kueleza kuwa, kiwango cha sasa cha naira 30,000 sawa na dola 22 kwa mwezi hakiwezi kukidhi mahitaji yao.
Kampuni ya kusambaza umeme Nigeria, TCN imeeleza katika taarifa kuwa wanachama wa muungano wa vyama vya wafanyikazi waliwafukuza wahudumu katika kituo kikuu cha kusambaza umeme na kuzima mitambo sita ya kusambaza umeme na kulitumbukiza taifa kwenye kiza kuanzia saa nane na dakika 19 usiku wa kuamkia leo.
Nalo shirika la ndege la Nigeria la Ibom Air limesema linasitisha safari zake za ndege kutokana na mgomo huo huku shirika lingine la United Nigeria likiweka wazi kuwa viwanja vyote vya ndege nchini humo vimefungwa na kwamba wafanyikazi waliogoma wamesema hawatoruhusu safari zozote za ndege.
Alice Joseph, ni mmoja wa wafanyikazi katika uwanja wa ndege wa Abuja.
"Chama cha wafanyikazi cha NLC kinatekeleza haki yake kwa sababu hali ya maisha imekuwa ngumu. Vitu ni ghali mno, kwa hivyo lazima wafanye kitu ili serikali ione na ishughulikie baadhi ya masuala yanayoibuliwa na kufanya watu waishi vizuri."
Ama kwa upande mwengine, vyama vya wafanyikazi wa kampuni ya kusambaza umeme na wafanyikazi wa uwanja wa ndege wamewaagiza wanachama wao kusitisha kutoa huduma kama sehemu ya kuitikia mgomo huo wa taifa.
Kadhalika wafanyikazi katika viwanda vya mafuta pia wameweka chini vifaa vyao vya kazi na kuapa kusitisha usambazaji wa mafuta. Hata hivyo mkuu wa shirika la mafuta la kitaifa Gbenga Komolafe amesema kunafanyika mipango ili kuhakikisha usambazaji wa mafuta hautatizwa na mgomo unaoendelea.
Soma pia: Nigeria inapata hasara kwa wizi wa mafuta
Muungano wa vyama vya wafanyikazi uliitisha mgomo wa kitaifa siku ya Ijumaa baada ya mazungumzo juu ya kiwango kipya cha mshahara wa chini kukosa kuzaa matunda. Muungano huo umesisitiza kuwa kamwe hawatolegeza kamba hadi pale matakwa yao yatakapozingatiwa.
Tangu aingie madarakani, Rais Tinubu amefanya mageuzi makubwa ambayo yamechochea kupanda kwa mfumuko wa bei na pia kuongezeka kwa gharama ya maisha.
Kiongozi huyo amekuwa kwenye shinikizo kutoka kwa muungano wa vyama vya wafanyikazi kuweka mikakati ya kupunguza gharama ya maisha na kusaidia kuinua biashara za wafanyibiashara wadogo wadogo hasa baada ya kuondoa ruzuku ya mafuta ya petroli ambayo ilisaidia mafuta kupatikana kwa bei nafuu.
Hata hivyo, ruzuku hiyo iliigharimu serikali kiasi dola bilioni 10 kwa mwaka.