Watoto 876 waachiwa huru kutoka kambi ya jeshi ya Giwa
29 Oktoba 2016Umoja wa Mataifa umesimamia mazungumzo ya kuachiwa mwaka huu watoto 876 waliokuwa wakishikiliwa katika kambi za wanajeshi wa Nigeria wakizuiliwa kama washukiwa wanaofungamana na kundi la itikadi kali la Boko Haram limeeleza shirika linaloshughulikia masuala ya watoto la Umoja huo Unicef.
Shirika hilo linakhofu kwamba mamia zaidi ya watoto bado wanashikiliwa katika kambi za jeshi kaskazini mashariki mwa mji wa Maiduguri ameliambia shirika la habari la Associated Press msemaji wa UNICEF tawi la Nigeria Doune Porter.Hii ni mara ya kwanza Umoja wa Mataifa unaripoti kuhusu kuhusika kusimamia mashauriano ya kuachiwa watoto hao ingawa jeshi la Nigeria mara kadhaa limesharipoti kuhusu ni watoto wangapi chini ya umri ni miongoni mwa waliookuwa wakishikiliwa wameachiwa huru baada ya kuwahoji na kusema kwamba limegundua kwamba watoto hao hawana mafungamano na kundi la Boko Haram.
Kiasi ya watoto kati ya hao 876 walioachiwa mwezi Desemba wamekuwa wakiishi katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa kundi la Boko Haram na walikamatwa baada ya maeneo hayo kukombolewa kwa mujibu wa Manuel Fontaine ambaye ni mkurugenzi wa UNICEF Afrika Magharibi na eneo la Kati.Porter ameeleza kwamba wengi wa watoto walioachiwa huru walikuwa ni chini ya umri wa miaka 5 na wengine walikuwa wangali wakinyonyeshwa na walikamatwa kwasababu wazazi wao walikuwa wakishukiwa .
Jeshi la Nigeria na polisi mara kwa mara wamekuwa wakiwafungia watoto sambamba na wazazi wao wakishukiwa kuwa wahalifu.Katika hatua pekee ya kuachiwa watoto hao iliyosimamiwa na UNICEF 560 waliachiwa mwezi Septemba ikiwemo watoto 430 wengine wakiwa na mama zao.Waliokamatwa wamekuwa wakizuiliwa katika mji wa Maiduguri mji ambao ni kitovu cha kundi la Boko Haram na ambako kuna kambi ya jeshi la Nigeria ya Giwa.
Wote waliokamatwa katika kambi hiyo wanashikiliwa kwasababu wanatuhumiwa kuunga mkono kundi la Boko Haram.
Shirika la habari la AP limehifadhi ushaihidi wa vifo vya maelfu ya wafungwa kutokana na hali mbaya ya mazingira ya usafi,msongamano na hali mbaya ya kibinadamu katika kambi hiyo ya Giwa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema wafungwa 8000 walifariki katika kambi hiyo kati ya mwaka 2011 na 2015.
Mwaka huu shirika hilo limetowa mwito wa kufungwa kwa vituo vyote vya kuwashikilia wafungwa likisema watoto wachanga na waliochini ya umri ni miongoni mwa wafungwa wengi wanaokufa kutokana na maradhi,njaa,ukosefu wa maji mwilini pamoja na kukosa kutibiwa majeraha ya risasi.
Mwandishi:Saumu Mwasimba/dpa/ap
Mhariri:Mohammed Dahman