1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia ya wagonjwa waondoka hospitali ya Al-Shifa

18 Novemba 2023

Shirika la Madaktari wasio na mpaka, MSF limesema wafanyakazi wake pamoja na familia zao wamenaswa katika eneo lililo karibu na hospitali ya Al-Shifa ambalo kwa siku kadhaa limekuwa chini ya udhibiti wa jeshi la Israel.

https://p.dw.com/p/4Z8Nu
Ukanda wa Gaza | Wapalestina waliojeruhiwa baada ya shambulizi la Israel
Wahanga wa mashambulizi ya IsraelPicha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Limesema watu 137, 65 kati yao wakiwa ni watoto wameshindwa katika juhudi zao za kulihama eneo hilo. MSF imetoa wito wa kusitishwa mapigano kati ya Israel na Hamas, ili raia waweze kuondoka, na limeonya pia kuwa uhaba wa chakula na maji unaweza kusababisha vifo.

Wakati huo huo, mamia ya wagonjwa,wauguzi na raia waliokuwa wakitafuta hifadhi katika hospitali ya al-Shifa ambayo ni kubwa zaidi katika Ukanda wa Gaza, wameondoka na kuhamia karibu na ufukwe wa bahari.

Shirika la habari la AFP limesema limeuona msururu wa wagonjwa, wakiwamo waliokatwa viungo vya miili, wakiondoka katika hospitali hiyo.

Jeshi la Israel limesema leo Jumamosi kuwa mkurugenzi wa hospitali ya al-Shifa aliomba njia salama ya kuwawezesha wagonjwa kuondoka, lakini Medhat Abbas, msemaji wa wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, amesema kuwa Israel ilitoa muda wa saa moja tu kwa wagonjwa wote kuondolewa katika hospitali hiyo.