1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Tanzania aliyeshikiliwa mateka na Hamas afariki

18 Novemba 2023

Raia mmoja wa Tanzania aliyetoweka tangu uvamizi wa kundi la wanamgambo wa Hamas kusini mwa Israel Oktoba 7, amethibitishwa kufariki dunia.

https://p.dw.com/p/4Z83I
Picha ya ishara I Waliotekwa na Hamas
Picha za wanaoshikiliwa mateka na HamasPicha: Petros Giannakouris/AP/picture alliance

Taarifa kutoka kwa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki imesema Mtanzania mwengine wa pili bado hajulikani alipo.

Taarifa hiyo iliyotolewa usiku wa kuamkia Jumamosi imesema kwamba familia ya mwanafunzi huyo wa kilimo Clemence Mtenga, imefahamishwa kuhusiana na kifo chake na mazungumzo kuhusu usafirishwaji wa mwili wake yanaendelea.

Tanzania inasema juhudi za kumtafuta raia wake wa pili Joshua Mollel zinaendelea. Haijawa wazi bado ni wapi mabaki ya Mtenga yalipopatikana ila wizara ya mambo ya nje inasema alikuwa miongoni mwa vijana 260 waliokuwa Israel kwa ajili ya kupata elimu ya kilimo.

Watu 240 walitekwa na kupelekwa Ukanda wa Gaza na wanamgambo wa Hamas, katika uvamizi uliochochea Israel kuanzisha vita dhidi ya kundi hilo ambavyo vimedumu kwa wiki sita sasa.

Hamas ambalo limeorodheshwa kama kundi la kigaidi na Ujerumani, Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine, liliwauwa raia 1,200 wa Israel wakiwemo wanajeshi.