Malori ya misaada ya WFP yawasili Gaza
13 Machi 2024Malori hayo ya misaada ya Mpango wa Chakula Duniani yamewasili kaskazini mwa Gaza huku kukiwa na tishio kubwa la njaa . WFP imesema imewasilisha chakula cha kutosha kwa watu 25,000 katika mji wa Gaza ikiwa ni msafara wa kwanza wenye mafanikio kuelekea eneo hilo tangu Februari 20 mwaka huu.
Jeshi la Israel (IDF) limesema lori hizo zilipitia barabara mpya ya kijeshi ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuzuia msaada huo kuangukia mikononi mwa kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Hamas ambalo Israel imesema inalenga kuharibu uwezo wa kijeshi wa kundi hilo.
Mashirika ya misaada yameonya kwamba Gaza inakabiliwa na njaa kutokana na vikwazo vya kuwasilishwa misaada. Meli ya misaada ya Uhispania ikitokea Cyprus pia iko njiani kuelekea Gaza.
Wakati huo huo, Ujerumani imetangaza kuwa inajiunga na nchi nyingine kadhaa ikiwa ni pamoja na Marekani na Ufaransa ambazo zimekuwa zikidondosha msaada kwa kutumia ndege kwenye eneo hilo la Wapalestina linalozingirwa na Israel la Ukanda wa Gaza.
Soma pia:Mashirika ya misaada yatahadharisha juu ya kuzuka baa la njaa kaskazini mwa Gaza
Hayo yakiarifiwa, Israel imeendeleza mashambulizi yake huko Gaza. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema moja ya ghala zake za usambazaji misaada huko Rafah limeshambuliwa na kusababisha vifo vya watu watano na uharibifu mkubwa. Mfanyakazi wa UNRWA Sami Abu Salim amesema:
" Tupo katika eneo linalolindwa kimataifa. Inakuwaje ndege za uvamizi zinaweza kulenga sehemu kama hii, sisi ni watu wasio na ulinzi wowote, tuko hapa kutoa misaada kwa watu walioyahama makazi yao kutoka kaskazini. Hili ni eneo la Umoja wa Mataifa na tulipaswa kufanya kazi hapa chini ya ulinzi wa Umoja wa Mataifa."
Idadi ya vifo yaongezeka Gaza
Wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas imesema hii leo kuwa hadi sasa watu 31,272 ndio tayari waliouawa tangu kuanza kwa mzozo huu Oktoba 7, 2023, wakati wapiganaji wa Hamas waliposhambulia kusini mwa Israel.
Wizara hiyo haitofautishi kati ya vifo vya raia na vya wapiganaji, lakini Umoja wa Mataifa na mashirika mengi ya kibinadamu yananasema idadi hiyo ya vifo ni ya kuaminika.
Soma pia:Vita vya Gaza vyatishia mzozo mkubwa Mashariki ya Kati
Aidha, mtu mmoja amearifiwa kuuwa baada ya Israel kushambulia gari moja kwa droni kusini mwa Lebanon. Shambulio hilo lilifanyika karibu na kambi ya wakimbizi wa KiPalestina ya Rashidiyah, karibu na mji wa Tyre. Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel amesema mtu huyo ni mwanachama mwandamizi wa Hamas aliyefahamika kama Hadi Ali Mustafa.
Hayo yanajiri siku moja tu baada ya Israel kusema kuwa imeyashambulia takriban maeneo 4,500 yenye mafungamano na kundi la Hezbollah katika nchi za Lebanon na Syria.
(Vyanzo: Mashirika)