Mali yakanusha uwepo wa mamluki wa Urusi
25 Desemba 2021Msemaji wa serikali Abdoulaye Maiga katika taarifa siku ya Ijumaa alikanusha kwamba askari wa kampuni binafsi ya usalama walikuwa wamepelekwa nchini Mali. Alisema "wakufunzi wa Urusi" walikuwa nchini humo kama sehemu ya makubaliano kati ya Mali na Urusi.
"inakanusha rasmi madai hayo yasio na msingi na matakwa kwamba ushahidi uletwe na vyanzo huru," Maiga alisema. "Wakufunzi wa Urusi wako nchini Mali kama sehemu ya kuimarisha uwezo wa operesheni za vikosi vya ulinzi na usalama vya taifa.
Haikubainika mara moja ni wepi wakufunzi hao wa Urusi, na jukumu lao hasa. Wizara ya utawala wa mikoa na ugatuzi haikuweza kupatikana kwa ajili ya kutoa ufafanuzi mapema Jumamosi.
Putin asema Wagner haiwakilishi taifa la Urusi
Mapema mwezi huu Umoja wa Ulaya ulisitisha ujumbe wake wa mafunzo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kwa sababu ya hofu kwamba ungehusishwa katika uvunjaji wa sheria ya kimataifa na mamluki wa Urusi, likiwemo kundi la Wagner.
Soma pia: Milipuko yatokea katika kambi ya UN nchini Mali
Marekani, ambayo iliiwekea vikwazo Wagner kutokana na matendo yake nchini CAR mapema mwaka huu, imekuwa ikikosoa mara kwa mara, uwezekano wowote wa kupeleka mamluki wa Urusi nchini Mali.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema upelekaji utaigharimu serikali ya Mali kiasi cha takribani dola milioni 10 kila mwezi na kuivuruga nchi hiyo wakati ikipambana kuzima uasi wa wapiganaji wa Kiislamu.
Soma pia:HRW: Mali sharti ichunguze madai ya mauaji
Rais wa Urusi Vladmir Putin amesema kundi la Wagner haliliwakilishi taifa la Urusi, lakini wakandarasi hao binfsi wa kijeshi wana haki ya kufanya kazi popote duniani ilimradi tu hawavunji sheria ya Urusi.
Chanzo: rtre