1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makundi 9 yaunda muungano kumpinga Abiy

5 Novemba 2021

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapanga kukutana leo Ijumaa kujadili hali nchini Ethiopia, ambapo mzozo kati ya serikali na waasi umekuwa ukiongezeka hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/42cVE
Äthiopien - Tigray-Truppen
Picha: picture alliance/AP

Makundi tisa yanayoipinga serikali nchini Ethiopia yakiwa yamekubaliana kuunda muungano dhidi ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed. 

soma Waziri mkuu Abiy aapa kuwazika maadui katika "damu yetu"

Makundi tisa yanayoipinga serikali nchini Ethiopia yamekubaliana kuunda muungano leo Ijumaa, katika tangazo lililoonekana na shirika la habari la Reuters wakati vikosi vya waasi vikisonga mbele kuelekea mji mkuu, Adis Ababa.

Miongoni mwa makundi hayo ni Jeshi la Ukombozi la Oromo (OLA) na Vuguvugu la Kidemokrasia la Agaw (ADM) na makundi mengine saba yaliyojiunga katika muungano huo pia yana wapiganaji wenye silaha kutoka maeneo mbalimbali ya taifa hilo.

Muungano huo uitwao United Front of Ethiopian Federalist na Confederation Forces, umejiunga na kikosi cha Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF ambao wamekuwa wakipambana na serikali ya Abiy Ahmed kwa mwaka mmoja katika vita ambavyo vimesababisha maelfu ya watu kuuwawa na kuwalazimisha zaidi ya milioni mbili kuyakimbia makaazi yao.

Wapinzani walikuwa na muda wa kutosha

Äthiopien | PK Billene Seyoum | Sprecherin des Premierministers
Billene SeyoumPicha: Yohannes Geberegziabher/DW

Msemaji wa Abiy, Billene Seyoum, alipoulizwa kuhusu muungano huo mpya unaoipinga serikali alitetea utawala wa Abiy kwa kusema kuwa kiongozi huyo alichukua madaraka mwaka wa 2018 baada ya wimbi la maandamano dhidi ya serikali na chama chake kilichaguliwa tena mwezi Juni.

Seyoum kupitia mtandao wa Twitter ameandika "Kufunguliwa kwa nafasi ya kisiasa miaka mitatu iliyopita kulitoa fursa ya kutosha kwa washindani kusuluhisha tofauti zao kwenye sanduku la kura mnamo Juni 2021.

Muungano huo unaundwa wakati mjumbe maalum wa Marekani Jeffrey Feltman yuko nchini Ethiopia kwa ajili ya kukutana na maafisa wakuu wa serikali, wakati ambapo wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja umetolewa na kutaka mazungumzo ya kumaliza vita hivyo. 

soma Wakaazi wa Addis Ababa watakiwa kusajili silaha zao

Kwa mujibu wa mratibu wa muungano huo mpya wa Yohanees Abraha kutoka kundi la TPLF, muungano wa United Front of Ethiopian Federalist Forces unataka kuanzisha mpango wa mpito nchini Ethiopia ili kumuondoa Waziri Mkuu Abiy Ahmed haraka iwezekanavyo.

Antony Blinken | US Außenminister
Antony Blinken Picha: Olivier Douliery/AP Photo/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken amesema mapigano nchini Ethiopia lazima yasitishwe na mazungumzo ya amani yanapaswa kuanza mara moja bila masharti yoyote.

soma Mashambulizi ya anga yautikisa mji mkuu wa Tigray

Kufuatia ombi kutoka kwa Mexico, wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanatarajiwa kushiriki mkutano huko New York. Kulingana na wanadiplomasia Baraza hilo lilikuwa linaandaa taarifa ya pamoja ingawa Urusi iliomba muda zaidi wa kufanya mashauriano.

Mapema hapo jana ubalozi wa Marekani mjini Addis Ababa uliidhinisha kuondoka kwa hiari kwa wafanyakazi wa ubalozi wasio wa muhimu na familia zao kutoka nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

 

Vyanzo; Reuters,dpa