Mashambulizi ya anga yautikisa mji mkuu wa Tigray
19 Oktoba 2021Awali serikali ya Ethiopia ilikanusha ripoti kuhusu mashambulizi ya anga katika mji huo na kuziita kuwa ni ''uongo mkubwa'' lakini baadaye shirika la habari la taifa lilithibitisha kuwa ndege za kijeshi zilikilenga chama cha ukombozi wa watu wa Tigray, TPLF.
Afisa wa ngazi ya juu katika hospitali kubwa zaidi jimboni Tigray amesema watu watatu waliuawa kwenye mashambulizi hayo wakiwemo watoto wawili. Haya ni mashambulizi ya kwanza ya anga katika mji wa Mekele tangu hatua za mwanzo za vita kaskazini mwa Ethiopia, machafuko ambayo yamesababisha mauaji ya watu wengi na mgogoro mkubwa wa kiutu.
Mashambulizi hayo ya mabomu ya yameripotiwa na wakaazi, maafisa wa mashirika ya wahisani na wanadiplomasia wakati serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed, ikionekana kuanzisha mashambulizi mapya dhidi ya chama cha TPLF. Chama hicho kimetawala siasa za taifa hilo kwa karibu miongo mitatu kabla ya Abiy kuingia madarakani mwaka 2018.
Shirika la habari la Ethiopia limesema mashambulizi ya anga ya hivi karibuni yalipiga pia vifaa vya mawasiliano na vyombo vya habari vilivyokuwa vikitumiwa na TPLF na kuongeza kuwa, hatua za kuzuia raia kujeruhiwa wakati wa mashambulizi hayo zilifanikiwa.
Umoja wa mataifa waonya
Umoja wa mataifa na Marekani, kwa pamoja zimetahadharisha kuhusu kuendelea kutokota kwa mzozo huo, na Stephen Dujarric msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa amezungumzia mashambulizi hayo ya hivi karibuni akisema kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ana wasiwasi mkubwa kuhusu kuzidi kukua kwa mgogoro Kaskazini mwa Ethiopia kama ilivyoonekana katika mashambulizi ya anga mjiini Mekele. Amesema katibu mkuu Guterres anasisitiza kuwa pande husika za mgogoro huo zinapaswa kuepuka kuwalenga raia ama miundombinu yao.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja, shambulio moja kati ya yaliyofanywa jana Jumatatu lilitokea karibu na kiwanda cha simenti, nje ya mji wa Mekele, unaodhibitiwa na TPLF tangu ulipotwaliwa kutoka kwa vikosi vya serikali mnamo mwezi Juni mwaka huu.
Shambulizi jingine linaripotiwa kuwa lilipiga katikati ya mji karibu na hoteli ya Planet ambayo mara nyingi hutumiwa na maafisa wa ngazi ya juu wa chama cha TPLF. Awali msemaji wa serikali alizitaja ripoti za mashambulizi hayo kuwa ni uzushi na kwamba zimesukwa na TPLF ili kuipotosha jamii ya kimataifa na kuongeza shinikizo kwa Ethiopia.