Marekani yatangaza kusitishwa mapigano kwa saa 72 Sudan.
25 Aprili 2023Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema baada ya mazungumzo katika muda wa saa 48 zilizopita, vikosi vya Wanajeshi wa Sudan vinavyopingana vya (SAF) kinachomtii Jenerali Abdel Fatah al Burhani na kikosi cha (RSF) kinachomtii Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo vimekubali kutekeleza amri ya kusitisha mapigano katika nchi nzima kuanzia usiku wa manane wa kuamkia leo Jumanne ambayo itadumu kwa saa 72.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani amesema nchi yake inashirikiana na washirika wake kuunda kamati ambayo itajadili usitishaji wa kudumu wa mapigano nchini Sudan.
Soma:Nchi za kigeni ziko mbioni kuwaokoa raia wao Sudan
Wakati ambapo serikali za kigeni zikiendelea na zoezi la kuwahamisha mamia ya wanadiplomasia wao pamoja na raia wao kuwapeleka mahala salama, Wasudan wanahangaika kutafuta njia za kuepuka machafuko hayo, wakihofia kwamba pande mbili za jeshi zinazopingana nchini humo zitazidisha vita vyao vya kuwania madaraka mara baada ya nchi za kigeni zitakapomilisha shughuli za kuwaondoa raia wao.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza wasiwasi juu ya mgogoro wa Sudan kugeuka na kuwa janga kubwa huku akiihimiza jamii ya kimataifa na nchi zenye nguvu kushinikiza upatikanaji wa amani nchini Sudan.
Guterres amesema mgogoro huo unaweza kusambaa kwenye eneo lote la Afrika. Akiwahutubia wajumbe 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Guterres alizitaka nchi wanachama wa baraza la usalama kutumia ushawishi wao ili kusitisha ghasia na kuirejesha Sudan kwenye mkondo wa kidemokrasia. Hotuba ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameitoa wakati ambapo Umoja huo ukiendelea na juhudi za kuwahamisha watu na kuwapeleka nje ya nchi hiyo inayokumbwa na mzozo.
Msafara wa Umoja wa Mataifa uliowabeba takriban watu 700 kutoka katika mapigano makali kwenye mji mkuu Khartoum hadi mji wa pwani wa Port Sudan, kwenye eneo la Bahari Nyekundukunakofanyika zoezi la kuwasafirisha watu ulikabiliwa na hali ngumu.
Soma:Papa Francis ahimiza mazungumzo kumaliza mzozo wa Sudan
Hata hivyo mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa,Volker Perthes amefahamisha kwamba watu wote walifika salama licha ya kutumia muda wa saa 35 katika msafara huo wa mikasa. Alisisitiza kwamba ni bora hivyo kuliko watu hao kukabiliwa na mapigano hata kwa saa tatu pekee.
Umoja wa mataifa umesema takriban watu 427 wameuawa mpaka sasa katika mapigano ya nchini Sudan yaliyoanza mnamo Aprili 15. Watu wengine 3700 wamejeruhiwa tangu mzozo huo ulipoanza.Baadhi ya hospitali zimeharibiwa kwenye mapigano hayo na maeneo mengine ya makazi yamegeuzwa kuwa maeneo ya vita.
Awali uwanja wa ndege wa Khartoum unaoripotiwa kuwa chini ya wapiganaji wa kikosi cha RSF kinachomtii Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo ulitajwa kuwa uwanja wa mapambano kati ya kikosi hicho na jeshi linalomtii Jenerali Abdel Fatah al Burhani.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema anawasiliana na pande mbili hizo zinazopingana nchini Sudan na amezitaka zisitishe mvutano na kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
Baraza la Usalama linapanga kufanya mkutano kuhusu Sudan leo Jumanne. Serikali ya Marekani imezitaka pande zinazopigana kuzingatia suluhu mara moja na kuhakikisha ulinzi wa raia.