Makubaliano ya kusitisha vita Gaza yanamalizika Jumatatu
27 Novemba 2023Makubaliano ya kusitisha vita yanaingia katika siku yake ya mwisho wakati Israel ikisema kuwa yanaweza kurefushwa kwa sharti la kuwaachilia mateka kumi kwa kila siku ya ziada ya kusitisha mapigano.
Kwa upande wake rais wa Marekani Joe Biden amesema kuwa madhumuni yake ni kuurefusha muda wa kusimamisha vita kwa kipindi kirefu kadri iwezekanavyo ili kuruhusu mateka wengi zaidi waachiliwe huru.
Soma zaidi: Qatar inatumai kurefushwa kwa usitishwaji mapigano kati ya Israel-Hamas
Nalo kundi la Hamas linalotizamwa na baadhi ya mataifa kama vile Israel Hamas, Ujerumani, Marekani na Umoja wa Ulaya kuwa la kigaidi limesema pia kuwa lipo tayari kurefusha muda wa kuweka chini silaha kama juhudi kubwa zitafanyika kuwaachilia huru Wapalestina wengi zaidi kutoka Israel. Hadi sasa wafungwa 100 wa Kipalestina wameachiliwa huru tangu makubaliano ya pande hizo mbili yalipoanza kutekelezwa.
Raia wa Thailand ni miongoni mwa mateka walioachiliwa Jumapili
Tukisalia katika mzozo huo, raia watatu wa Thailandni miongoni mwa mateka walioachiliwa katika siku ya tatu ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas.
Kulingana na kauli ya Waziri Mkuu wa Thailand Srettha Thasivin kupitia jukwaa la X, mateka hao wameachiliwa wakiwa na afya njema na kuwa hawahitaji huduma ya kidaktari. Ameongeza kuwa watu hao watarejeshwa Thailand mapema iwezekanavyo. Hadi sasa, raia 17 wa Thailand waliokuwa wakishikiliwa mateka na kundi la Hamas wamekwisha kuachiliwa.
Katika hatua nyingine, Jeshi la wanamaji la Marekani limesema limewakamata watu watano waliojihami kwa silaha katika Ghuba ya Aden baada ya kuikomboa meli ya Israel iliyokuwa imetekwa nyara. Kamandi kuu ya Marekani imesema wanamaji kutoka katika meli ya kijeshi ya Marekani walipokea mawasiliano yaliyoashiria tatizo kutoka kwenye meli iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Liberia baada ya wafanyakazi wake kuripoti kuwa ilikuwa imetekwa.