1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na Hamas wabadilishana mateka, wafungwa

25 Novemba 2023

Hamas imewaachia mateka 24 iliyowashikilia Gaza kwa wiki kadhaa, na Israel ikawaachia wafungwa wa Kipalestina kutoka jela katika awamu ya kwanza ya mabadilishano chini ya mpango wa usitishwaji mapigano kwa siku nne

https://p.dw.com/p/4ZQv4
Westjordanland | Ehemalige palästinensische Gefangene, die von den israelischen Behörden freigelassen wurden
Wafungwa wa Kipalestina walioachiwa kutoka magereza ya Israel wawasili Beituna, magharibi mwa RamallahPicha: Issam Rimawi/Anadolu/picture alliance

Wapiganaji wa Hamas wamewaachia huru mateka 24 siku ya Ijumaa katika siku ya kwanza ya kusitishwa vita hivyo kwa mara ya kwanza. Mateka hako walijumuisha wanawake na watoto na wafanyakazi wa Thailand na mmoja wa Ufilipino,baada ya silaha kunyamazishwa kwa mara ya kwanza kote Ukanda wa Gaza katika kipindi cha wiki saba.

Soma pia: Wapalestina waanza kurejea kwao baada ya mapigano kusimama

Mateka hao walihamishwa kutoka Gaza na kukabidhiwa maafisa wa Misri katika kivuko cha Rafah, wakiandamana na wafanyakazi wanane wa Shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu kwenye msafara wa magari manne.

Mateka walioachiwa huru Gaza wawasili Israel

Israel | on der Hamas freigelassene israelische Geiseln treffen in Petach Tikwa ein
Mateka walioachiwa huru wawawili Israel kwa helikoptaPicha: Ohad Zwigenberg/AP/picture alliance

Qatar, ambayo ilikuwa mpatanishi wa mpango huo wa kusitishwa vita, ilisema Waisrael 13 waliachiwa huru, baadhi wakiwa wenye uraia pacha. Wanawake na watoto 39 wa Kipalestina waliachiwa kutoka magereza ya Israel.

Miongoni mwa walioachiwa ni wafungwa waliokamatwa kwa makosa yakiwemo tuhuma za mashambulizi ya visu, kuwarushia mawe askari wa Israel au kuwa na mawasiliano na makundi ya uhasama. Katik mji wa Beituna wa Ukingo wa Magharibi, mamia ya Wapalestina walimiminika nje ya majumba yao kusheherekea, wakipiga honi na kufyatua fataki.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kuwaleta nyumbani mateka wote wanaoshikiliwa Gaza. Jeshi la Israel limesema raia hao walifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu ndani ya ardhi ya Israel kabla ya kupelekwa hospitali na kukutanishwa na familia zao. Msemaji wa jeshi lsrael Daniel Hagari amesema wote wako katika hali nzuri.

Biden akaribisha kuwachiwa mateka kutoka Gaza

Rais Joe Biden wa Marekani amesema kuwachiwa kwa mateka wa kwanza chini ya mpango kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Hamas ni mwanzo na akasema kuna nafasi halisi ya kuyarefusha makubaliano hayo huko Gaza.

Rais Joe Biden akizungumza Nantucket
Biden amesema anatarajia mateka zaidi kuwachiwaPicha: Stephanie Scarbrough/AP/picture alliance

Akizungumza na waandishi habari, Biden amesema wanatarajia mateka zaidi kuwachiwa huru leo, na wengine kesho na wengine siku inayofuata. Ameongeza kuwa ni wakati sasa wa kuanzisha upya kazi ya kuunda suluhisho la mataifa mawili kwa ajili ya amani kati ya Israel na Wapalestina.

Gaza yapokea msafara mkubwa zaidi wa misaada tangu Oktoba 7

Umoja wa Mataifa umesema malori 137 yaliyobeba msaada wa kiutu yaliingia katika Ukanda wa Gaza jana. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya msaada wa kibinaadamu – OCHA imesema kuwa wakati wa usitishwaji mapigano ambao ulianza jana asubuhi, Umoja wa Mataifa uliweza kuongeza upelekaji wa misaada ya kiutu ndani ya Gaza.

Imesema lita 129,000 za mafuta na malori manne yaliyobeba gesi pia yaliingia Gaza. Huo ndio msafara mkubwa kabisa wa misaada ya kiutu kuingia Gaza tangu Oktoba 7. Shirika hilo limesema mamia ya maelfu ya watu walipewa chakula, maji, bidhaa za matibabu na vifaa vingine muhimu vya kibinaadamu.

dpa