1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makabiliano makali yaendelea nje kidogo ya Kyiv

26 Februari 2022

Wanajeshi wa Urusi wameendeleza harakati zao kuelekea mji mkuu wa Ukraine, Kyiv baada ya usiku wa miripuko na mapambano ya mitaani kuwafanya wakazi kutafuta hifadhi katika mahandaki

https://p.dw.com/p/47eIJ
Ukraine - Kiew
Picha: Sergei Supinsky/AFP

 "Mapigano yako hapa,” Amesema Rais Volodymyr Zelensky. Haijafahamika wazi wanajeshi wa Urusi wamesogea kwa umbali gani. Maafisa wa Ukraine wameripoti mafanikio kadhaa katika kuzuia mashambulizi, lakini mapigano yameendelea karibu na mji mkuu. Makabiliano yaliyoripotiwa viungani mwa mji huo yaliashiria kuwa vikosi vidogo vya Urusi vinajaribu kusafisha njia kwa wanajeshi wao kuingia.

Soma pia: Rais wa Ukraine ahofia mji mkuu, Kiev kushambuliwa na majeshi ya Urusi awataka wananchi waulinde

Urusi inadai mashambulizi yake nchini Ukraine yanalenga maeneo ya kijeshi pekee, lakini raia wameuawa na kujeruhiwa kwenye vita hivyo vya karibuni kabisa vya ardhini tangu Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Ukraine Krieg l Präsident Selenskyi, Facebook Selfie
Rais Zelensky amesema Ukraine itapambanaPicha: FACEBOOK/@Volodymyr Zelensky/AFP

Kombora lilipiga jengo moja la makazi katika viunga vya kusini magharibi karibu na viwanja viwii vya ndege za abiria, amesema Meya Vitali Klitschko, na kusababisha uharibifu. Raia sita walijeruhiwa. Meya amerefusha amri ya kutotembea nje ya saa nne kamili usiku hadi saa moja kamili asubuhi aliyoiweka siku mbili zilizopita na sasa itaanza saa kumi na moja hadi saa mbili asubuhi kuanzia leo.

Soma pia: Wanajeshi wa Urusi waukaribia kabisa mji mkuu wa Ukraine Kiev

Mzozo huo tayari umesababisha mamia kwa maelfu ya Waukraine kutoka makwao. Umoja wa Mataifa umesema Zaidi ya Waukraine 120,000 wameondoka nchini na kuingia Poland, Moldova na mataifa mengine jirani.

Wizara ya ulinzi ya Urusi imedai kuwa jeshi la Urusi limechukua udhibiti kamili wa mji wa Melitopol kilomita 35 kutoka pwani ya Bahari ya Azov, na wapiganaji wanaoungwa mkono na Urusi wamekamata maeneo mengi ya mkoa wa mashariki wa Donbas.

Polen | Ukrainische Flüchtlinge am Grenzübgang Korczowa
Maelfu ya Waukraine wanaingia nchi jiraniPicha: Czarek Sokolowski/AP Photo/picture alliance

Soma pia: Vikwazo vipya dhidi ya Urusi ni vikali kiasi gani?

Maafisa wan chi za Magharibi wanaamini Rais wa Urusi Vladmir Putin amedhamiria kuiangusha serikali ya Ukraine na kuuweka utawala wake mwenyewe.

Zelensky amesisitiza leo kuwa jeshi la nchi yake litakabiliana na uvamizi huo wa Urusi. Amerekodi video akimuonyesha akiwa mjini Kyiv, akisema bado yuko mjini humo na kuwa madai ya jeshi la Ukraine kuweka chini silaha ni za uwongo.

Waziri wa afya wa Ukraine amesema leo kuwa watu 198 wakiwemo Watoto watatu, wameuawa na Zaidi ya 1,000 kujeruhiwa tangu kuanza uvamizi wa Urusi wa angani, ardhini na majini Alhamisi. Maafisa wa Ukraine wamesema mamia ya Warusi wameuawa katika siku za kwanza za mapigano hayo. Serikali ya Urusi haijatoa idadi yoyote ya wahanga.

Marekani na madola mengine yenye nguvu duniani wamezuia mali za Putin na waziri wake wa mambo ya kigeni Sergei Lavrov kama sehemu ya vikwazo vikali dhidi ya Urusi. Urusi hata hivyo haitishiki na vikwazo hivyo na imechukua hatua ya kulipiza kisasi kwa kutangaza vikwazo dhidi ya nchi hizo.

ap, reuters, dpa, afp