1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Urusi waukaribia kabisa mji mkuu wa Kiev

25 Februari 2022

Urusi yadai imeshauteka uwanja wa ndege muhimu unaoiunganisha Kiev na nchi za Magharibi na itautumia kusafirisha haraka wanajeshi wake kuingia kwenye mji huo

https://p.dw.com/p/47cO6
Ukraine Konflikt | Russischer Militäreinsatz
Picha: Sergei Malgavko/ITAR-TASS/imago images

Wanajeshi wa Urusi leo Ijumaa wanaukaribia mji mkuu wa Ukraine, Kiev, zikikisikika sauti za  milio ya risasi na miripuko karibu kabisa na majengo ya shughuli za kiserikali.

Huu ni uvamizi wa Urusi katika nchi yenye kuzingatia mifumo ya kidemokrasia na ambao umeongeza khofu ya kutokea vita vipana katika bara la Ulaya na kuchochea pia juhudi za ulimwengu za kutaka kuizuia Urusi.

Ukraine | Menschen in Kiew suchen Schutz in Metro-Stationen
Picha: Zoya Shu/AP/dpa/picture alliance

Kufuatia kuongezeka idadi ya waliokufa kutokana na hujuma ya Urusi ambayo imejumuisha mashambulizi ya makombora dhidi ya majumba, madaraja na shule katika maeneo ya Kiev, serikali ya Urusi imesema nchi yake iko tayari kuzungumza na maafisa wa Ukraine.

 Na msimamo huu umekuja katika wakati ambapo zimeonekana ishara zikiongezeka kwamba Rais Vladmir Putin huenda anataka hasa kuiondowa kwa nguvu madarakani serikali ya Rais Volodymyr Zelensky, hatua ambayo inatazamwa kama juhudi kubwa za Urusi za kutaka kuichora upya ramani ya dunia na kufufua upya ushawishi wake wa enzi ya Vita Baridi.

Marekani na nchi nyingine zenye nguvu duniani wameiwekea vikwazo vikali kabisa Urusi na uvamizi wa Urusi unaweza kuiongezea hata zaidi nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi na usambazaji wa nishati, na kutishia kutokea hali mbaya zaidi ya kuwaumiza wananchi wa kawaida wa Urusi.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema wanaandaa hatua za kuwezesha mamilioni ya wananchi kuondoka Ukraine.

Lakini pia viongozi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO wameitisha mkutano wa dharura kujadili namna ya kutazama ni kwa umbali gani wanaweza kumzuia Putin bila ya kulihusisha jeshi la Urusi kwenye vita ya moja kwa moja.

Ukraine | Menschen auf dem Weg zu Zügen um Kiew zu verlassen
Picha: Emilio Morenatti/AP/dpa/picture alliance

Uvamizi wa Urusi ulioingia siku yake ya pili umeelekezwa zaidi katika mji mkuu Kiev ambako waandishi habari wa shirika la Associated Press wamesema wamesikia miripuko kuanzia alfajiriya  Ijumaa na sauti za milio ya risasi katika maeneo chungu nzima.
 

Ukraine yajitetea

Maafisa wa Ukraine wametumia magari ya kijeshi pamoja na magari ya kuzowa theluji kuulinda mji wa Kiev na kuzuia watu kutembea. Lakini pia maafisa wa Ukraine wamesema majasusi wa Urusi wanahangaika kutafuta namna ya kuingia katika mji huo.

Jeshi la Urusi limesema limeshaudhibiti uwanja muhimu wa ndege wa kimkakati ulioko nje ya Kiev ambao unaiwezesha nchi hiyo kupeleka haraka wanajeshi wake katika mji mkuu, Kiev.

Ukraine Konflikt | Präsident Volodymyr Zelenskyy
Picha: Ukrainian Presidential Press Office/AP Photo/picture alliance

Kadhalika Urusi imedai kwamba tayari imeshautenganisha mji huo na nchi za Magharibi kwa maana ya kuyadhibiti maeneo mengi ambayo ni njia wanayoelekea watu wengi wanaokimbia uvamizi, huku misururu ya magari ikionekana ikielekea eneo la mpakani na Poland.

Rais Zelensky hajulikani aliko

Inaelezwa kwamba aliko Rais Zelensky ni suala lililowekwa siri baada ya mwenyewe kuwaambia viongozi wa Umoja wa Ulaya kwamba ni mtu wa kwanza katika orodha ya watu wanaolengwa na Urusi.

Japokuwa rais huyo ametoa pendekezo la kutaka mazungumzo na Urusi kuhusu madai muhimu yaliyotakiwa na Moscow, ambayo ni kuitaka Ukraine itangaze kuwa haina upande na itaaachana na dhamira yake ya kutaka kujiunga na NATO.

Urusi kwa upande wake imejibu pendekezo hilo ikisema iko tayari kutuma ujumbe wake nchini Belarus kuyazungumza hayo.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Khelef

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW