Mahakama Ujerumani yakosoa mageuzi ya sheria ya uchaguzi
30 Julai 2024Matangazo
Mageuzi hayo, yaliyopendekezwa na serikali ya mseto ya kansela Olaf Scholz, yanalenga kupunguza ukubwa wa bunge la Ujerumani Bundestag liwe na viti 630. Idadi ya sasa ya wabunge katika bunge hilo ni 733 kutokana na mfumo wa upigaji kura unaowapa viti washindi wa kura za maeneo ya uwakilishi, pamoja na viti vinavyopewa kila chama kulingana na idadi ya kura vilizoshinda kitaifa.
Chama cha kihafidhina cha Christian Social Union, CSU na chama cha mrengo mkali wa kushoto cha Die Linke vilikuwa vimewasilisha rufaa katika mahakama ya katiba mjini Karlsruhe kuhusu mageuzi hayo yaliyopitishwa na baraza la chini la bunge la Ujerumani mnamo Machi 2023. Vyama hivyo viliyapinga mageuzi hayo vikisema si ya haki kwao.