Mahakama Uganda yasimama na sheria ya kupinga ushoga
3 Aprili 2024Mahakama ya Katiba nchini Uganda leo imelikataa ombi la kuipindua sheria yenye utata ya kupinga mapenzi ya jinsia moja, inayochukuliwa kama mojawapo ya sheria kali zaidi duniani.
Akisoma uamuzi huo, Hakimu Richard Buteera ambaye pia ni naibu jaji mkuu wa Uganda na mkuu wa mahakama hiyo ya katiba amesema, sheria hiyo haitofutiliwa mbali na hakutatolewa agizo la kupinga utekelezaji wake.
Sheria hiyo ilipitishwa Mei mwaka jana na kusababisha ghadhabu miongoni mwa jamii yawapenzi wa jinsia moja, wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi.
Sheria hiyo inatoa adhabu ya hadi kifungo cha maisha kwa watu walio katika mahusiano ya jinsia moja na ina vipengee vinavyoufanya ushoga kuwa kosa linaloweza kuadhibiwa kwa adhabu ya kifo.
Serikali ya Rais Yoweri Museveni imeitetea sheria hiyo ikidai mataifa ya Magharibi yanaishinikiza Afrika ikubalia mapenzi ya jinsia moja.