1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yatinga robo fainali AFCON kwa kuipiga Kamerun 2-0

28 Januari 2024

Ademola Lookman alifunga mabao yote mawili Nigeria ilipowashinda wapinzani wake wa zamani Kamerun magoli 2-0 Jumamosi na kutinga robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

https://p.dw.com/p/4blOz
 Ivory Coast | AFCON | Nigeria
Wachezaji wa Nigeria wakishangilia ushindi.Picha: Franck Fife/AFP

Bao la mapema la Nigeria lililofungwa na Semi Ajayi lilikataliwa kufuatia uchunguzi wa teknolojia ya VAR katika pambano hilo la hatua ya 16 kabla ya shinikizo mfululizo dhidi ya safu ya ulinzi wa Kamerun na Victor Osimhen kupelekea Lookman kuzifumania nyavu dakika ya 36.

Nigeria, timu ambayo imekuwa ngumu kufungwa katika AFCON ya mwaka huu iliwadhibiti Indomitable Lions kabla ya Lookman kuhakikisha ushindi katika dakika ya 90 mbele ya mashabiki 22,085 kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny mjini Abidjan.

Sasa watarejea uwanjani hapo kwa ajili ya mechi ya nane bora Ijumaa ijayo dhidi ya Angola, ambayo awali iliishinda Namibia 3-0. "Ilikuwa ni kiwango kikubwa kilichoonyeshwa na timu, tulipambana vyema kuanzia dakika ya kwanza hadi ya 100,” alisema Lookman.

Ikiwa na Osimhen akiongoza kutoka mbele, Super Eagles ni tishio kubwa kwa mabingwa watetezi Senegal wanaposaka taji la nne la bara la Afrika.

"Nina furaha sana na vijana wangu. Nafikiri timu yetu ilifanya kazi nzuri sana dhidi ya timu nzuri sana. Tulistahili kushinda," alisisitiza kocha wa Nigeria Jose Peseiro.

Victor James Osimhen - Kombe la Mataifa ya Afrika
Nyota wa Nigeria James OsimhenPicha: BackpagePix/empics/picture alliance

Wakati huo huo, kocha wa Kamerun Rigobert Song alisema ukosefu wa uzoefu uliigharimu timu yake inaporejea nyumbani. "Nina timu changa na wachezaji ambao wanajifunza katika kiwango hiki," alikiri.

"Watajifunza na kuimarika kutokana na makosa yao. Katika miaka miwili au mitatu kuanzia sasa watakuwa wachezaji wale wale lakini timu tofauti."

Ratiba hii ni mfano bora wa Kombe la Mataifa, ambapo mataji matatu ya kwanza kati ya matano waliyoyashinda Kamerun yalikuja baada ya kuishinda Nigeria kwenye fainali.

La kwanza kabisa, wakati timu inayoongozwa na Roger Milla ilipotoka nyuma na kushinda 3-1 mwaka 1984, lilipatikana katika uwanja huu huu ulioko mji mkuu wa kiuchumi wa Ivory Coast.

'Lengo ni kutoruhusu kabisaa magoli'

Hata hivyo Nigeria ilishinda pambano la karibuni zaidi dhidi ya majirani zao, katika hatua ya 16 bora nchini Misri miaka mitano iliyopita, na timu yao ya sasa iliingia katika mechi hii ikipewa nafasi bora zaidi ya kuibuka mshindi.

Super Eagles walifuzu kwa urahisi katika kundi lao bila kushindwa, huku Kamerun wakihitaji bao la dakika za lala salama dhidi ya Gambia ili kusonga mbele.

Jina lao linalotambulika zaidi ni Andre Onana, lakini mlinda mlango huyo wa Manchester United alitemwa kwa mara ya pili mfululizo, huku Fabrice Ondoa wa timu ya daraja la tatu ya Ufaransa Nimes akipendelewa kusimama golini.

Kocha ya Timu ya Taifa ya kamerun - Rigobert Song Bahanag
Kocha ya Kamerun Rigobert Song Bahanag amesema vijana wake hawakuwa na uzoefu wa kutosha kukabiliana na Nigeria.Picha: Lee Jin-man/AP/picture alliance

Vincent Aboubakar, nahodha wao na tishio kuu kwa walinda mlango, alitajwa miongoni mwa wachezaji wa akiba baada ya kukosa kucheza hatua ya makundi.  

Soma pia: Taifa Stars yatupwa nje ya michuano ya AFCON

Nigeria ilimrejesha nahodha William Troost-Ekong, Lookman na Alex Iwobi -- mfungaji wa bao la ushindi katika mechi hiyo ya 2019 -- baada ya wote kupumzishwa kwa mechi yao ya mwisho dhidi ya Guinea-Bissau.  Mechi hiyo iliisababishia Kamerun matatizo tangu mwanzoni, na Nigeria walidhani walichukua uongozi ndani ya dakika nane.

Shuti la Moses Simon liliokolewa na Ondoa lakini mpira ukamuangukia Ajayi na beki wa West Bromwich Albion akatikisa wavu licha ya mlinda mlango kuugusa. Vifijo na nderemo vilifuatia, kabla ya muamuzi wa Morocco kushauriana na timu ya teknolojia ya VAR na kulifuta bao hilo, kwa sababu Ajayi alionekana kuwa ameotea.

Bila kukatishwa tamaa, Nigeria haikuacha kushambulia, huku Osimhen asiyechoka akitoa mfano. Alichochea bao la ufunguzi, kwa kumpokonya Oumar Gonzalez baada ya mpira wa kurushwa uliochezwa na beki wa Kamerun, na kisha akamtengezea Lookman bila ubinafsi.

Kombora la fowadi huyo wa Atalanta lilimlenga Ondoa moja kwa moja, lakini kipa huyo aliweza kuusaidia tu mpira kutua golini. Osimhen alianguka uwanjani kwenye kipenga cha mapumziko, lakini mwanasoka huyo bora wa mwaka wa Afrika alipata tena nguvu baada ya kuanza kwa kipindi cha pili.

Michuano ya AFCON 2024 yaanza Ivory Coast

Peseiro amesisitiza kuwa kipaumbele cha timu yake ni kuhakikisha hawaruhusu mabao, na walisimama kidete licha ya kwamba kipa Stanley Nwabili kutolewa nje kwa machela.

Kuingizwa kwa Aboubakar kwa upande wa Kamerun hakukubadili chochote, na Nigeria ikapata bao la pili kabla ya mchezo kuhamia dakika 10 za majeruhi.

Calvin Bassey alipiga mkwaju wa chini kutokea upande wa kushoto na Lookman, mzaliwa wa London akamilizia.