1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya Wairan wamuaga kamanda Soleimani

6 Januari 2020

Kiongozi wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameongoza maelfu ya watu katika mji mkuu wa Iran, Tehran katika shughuli ya mazishi ya kamanda mwandamizi wa jeshi Qassem Soleimani.

https://p.dw.com/p/3VlJ0
Iran Trauerzeremonie für getöteten General Soleimani in Teheran |
Picha: AFP/Office of Iran's Supreme Leader Ayatollah Ali Khamenei

Sauti ya Khamenei ilikwama kwa kipindi kifupi kutokana na machungu wakati kiongozi huyo alipokuwa akiongoza shughuli hiyo ya umma huku akishindwa kuzuia machozi.

Kulingana na televisheni ya umma nchini Iran, mamilioni ya raia wamejitokeza kwenye mitaa ya mji mkuu Tehran kutoa heshima zao za mwisho kwa kamanda huyo wa kikosi maalumu cha al-Qudskinachohusika na operesheni za kijeshi za nje.

Mkusanyiko huo unatajwa kuwa ni mkubwa zaidi wa mazishi tangu ule wa mwaka 1989 wa mazishi ya mwasisi wa taifa hilo la Kiislamu Ayatollah Ruhollah Khomenei, aliyeongoza mapinduzi yaliyoibua makwaruzano ya kisiasa na Marekani. Wengi wa wairan wanamuona Soleimani kama shujaa wa kitaifa na aliyechukuliwa kama mtu wa pili kwa mamlaka makubwa zaidi nchini humo baada ya Khamenei.

Umati katika mkusanyiko huo ulipaza sauti ukisema, "kifo kwa Marekani" na muombolezaji mmoja alibeba bango lililoandikwa "tuna haki ya kulipiza kisasi kikali", matamshi ambayo awali yalitamkwa na viongozi wa kijeshi na kisiasa wa Iran.

Iran Trauerzeremonie für getöteten General Soleimani in Teheran | Ayatollah Ali Khamenei
Ayatollah na viongozi wenzake walishindwa kujizuia kutoa machozi wakati wa shughuli hiyo ya kumuaga SoleimaniPicha: picture-alliance/AP Photo/Iran Press TV

Mwanaye wa kike Zeinab Soleimani amesema kwenye shughuli hiyo ya mazishi katika chuo kikuu cha Tehran kwamba, familia ya wanajeshi wa Marekani nazo zisubiri kushuhudia vifo vya wapendwa wao, alisema "Familia ya wanajeshi wa Marekani kwenye eneo la Asia Kaskazini zimeshuhudia mateso ya Marekani katika vita vya Syria, Iraq, Lebanon, Afghanistan na Palestina na wao wasubiri kushuhudia vifo vya vizazi vyao"

Baadhi ya mataifa yaziomba Iran na Marekani kujizuia.

Nchini Ujerumani waziri wa mambo ya kigeni Heiko Maas amesema tangazo la Iran hapo jana  la kuachana na ukomo wa urutubishaji wa madini ya urani, huenda ikawa ni hatua ya awali kuelekea mwisho wa mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 iliokubaliana na mataifa sita yenye nguvu duniani.

Matangazo ya asubuhi 01.06.2019

Ingawa Iran ilitarajiwa kutoa tangazo hilo mwishoni mwa wiki lakini wakati ambapo tangazo hilo limetolewa unahusishwa na mzozo unaozidi kufukuta kati ya Marekani na Iran hasa kufuatia mauaji dhidi ya Soleimani. Maas amekiambia kituo cha radio cha Ujerumani cha Deutschlandfunk kwamba watazungumza tena na Iran kwa kuwa hatua hiyo inapingana na makubaliano hayo.

China yenyewe imeikosoa Marekani kwa kuchochea mzozo kwenye ukanda wa Mashariki ya Kati, kufuatia matumizi yake ya nguvu katika mvutano kati yake na Iran huku ikizitaka pande zote mbili kujizuia na kuhakikisha kunakuwepo amani na utulivu. 

Afrika Kusini nayo imelaani mashambulizi hayo ya Marekani iliyoyaita "ugaidi wa kimataifa" huku ikitaka kujizuia. Taarifa yake imeonekana kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook mwishoni mwa wiki iliyotolewa na katibu mkuu wa chama tawala, ANC Ace Magashule. Wizara ya mambo ya nje aidha, imetoa taarifa ndefu zaidi inayounga mkono uhuru wa Iraq na kutoa mwito wa mazungumzo na utulivu.