1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano pale pale licha ya mazungumzo

7 Februari 2011

Rais Hosni Mubarak anakabiliwa na shinikizo jipya la kumtaka aondoke madarakani, baada ya wapinzani kusema kwamba mazungumzo yao na serikali hapo jana hayajaweza kufanikiwa kuzima maandamano yao dhidi ya kiongozi huyo.

https://p.dw.com/p/10Bw3
Waandamanaji na mabango ya Kihibru na Kiarabu
Waandamanaji na mabango ya Kihibru na KiarabuPicha: AP

Wakati jua la siku ya leo lilipochomoza, maelfu ya waandamanaji ambao wamekuwa wakilalia na kuamkia uwanja wa Tahrir, walijitoa kwenye mablanketi yao na kuanza kupiga tena kelele za kumtaka Rais Mubarak aondoke.

Wengi wao walikuwa wamelala chini ya vifaru vya jeshi, vilivyojazana kwenye uwanja huo, wakikhofia kwamba wakiviwacha peke yao, vingekuja kuondoka usiku na kuwaruhusu wafuasi wa Mubarak kuwashambulia, kama ilivyotokea wiki iliyopita, ambapo zaidi ya watu 15 walipoteza maisha na mamia kujeruhiwa.

Hapana kuaminiana

Muandamanaji aliyejichora "Mubarak Ondoka!"
Muandamanaji aliyejichora "Mubarak Ondoka!"Picha: DW

Leo serikali ya Misri inafanya kikao chake cha kwanza cha baraza la mawaziri, tangu lilipoundwa upya na Rais Mubarak, kufuatia maandamano yanayoendelea dhidi yake. Lakini, inavyoonekana muhanga mkubwa wa mgogoro huu wa Misri ni imani baina ya waandamanaji na serikali yao.

Hata baada ya hatua kadhaa zilizochukuliwa na serikali, ikiwamo ya mazungumzo ya jana kati ya Makamo wa Rais Omar Suleiman na makundi ya upinzani juu ya kuumaliza mkwamo wa kisiasa, bado waandamanaji na viongozi wa upinzani, hawaonekani kuwaamini watawala, seuze kuwatii.

Hata hivyo, msemaji wa serikali Magdi Radi, amesema kwamba, katika mazungumzo ya jana, serikali na wapinzani waliafikiana kuunda kamati ya wataalamu wa sheria na wanasiasa ya kupendekeza na kuzingatia mabadiliko ya katiba yanayohitajika hadi kufikia mwanzoni mwa mwezi ujao.

Maafikiano ya awali

Bango
BangoPicha: DW

Maafikiano pia yalikuwa juu ya kufunguliwa kwa ofisi maalum ya kusajili malalamiko ya mateso dhidi ya wafungwa wa kisiasa, kuondosha vikwazo kwa vyombo vya habari, kuondoa sheria ya hali ya dharura, ambayo Mubarak amekuwa akiitumia tangu aingie madarakani miaka 30 iliyopita na kukataa uingiliaji kati kutoka nje.

Kundi la Ikhwanul-Muslimin, Udugu wa Kiislamu, ambalo lina nguvu zaidi miongoni mwa makundi ya upinzani nchi humo, limerejelea matakwa ya kwanza Mubarak kuwachia madaraka mikononi mwa makamo wake, ndipo mazungumzo yaendelee.

Lakini wengi wanaamini kuwa, si makamo wa Rais Omar Suleiman, wala waziri mkuu Ahmed Shafiq, mwenye ubavu wa kumuambia Mubarak aondoke, hata kama wangelitaka iwe hivyo.

Msemaji wa Ikhwanul-Muslimin, Mahmud Ezzat, Essal El-Erian, anasema wao wanajua kuwa bado safari ya kufikia mageuzi ingalipo.

"Bila ya shaka, tunajuwa kuwa itachukua muda kuubadilisha utawala. Haigharimu kitu sana kwa Mubarak kuondoka, ni jambo la saa, au wiki, lakini kuubalisha utawala wake na kuwa na uchaguzi huru na wa haki kutachukuwa muda, labda miezi sita ya kipindi cha mpito." Amesema El-Erian.

Wasiwasi wa kushiriki Ikhwanul-Muslimin

Muandamanaji wa Ikhwanul-Muslimin
Muandamanaji wa Ikhwanul-MusliminPicha: AP

Lakini, kushiriki kwa Ikhwanul-Muslimin kwenye mazungumzo haya, kumepokewa kwa hisia mchanganyiko katika mataifa ya Magharibi, hasa Marekani, ambayo ni mshirika mkubwa wa Mubarak, ikikhofiwa kwamba ushawishi wa kundi hilo kwenye siasa za Misri unaweza kuipa tabu Israel hapo baadaye.

Rais Barack Obama, ambaye mwanzoni alikuwa na kauli za wazi na nzito kuhusiana na uwezekano wa Mubarak kuondoka, sasa ameanza kubadilisha mahadhi ya sauti yake, akisema kwamba, japokuwa muda wa mabadiliko ni sasa, lakini Ikhwanul-Muslimin haiwakilishi matakwa ya wengi.

Waziri wake wa Mambo ya Nje, Hilarry Clinton, amesema kwamba kuondoka na kutoondoka kwa Mubarak ni suala la kuamuliwa na Wamisri wenyewe, lakini akaonya kuwa uondokaji wa mapema unaweza kusababisha matatizo makubwa zaidi, hasa ikiwa wapinzani bado hawajajipanga.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman